Trump atoa radiamali kufuatia kuatunguliwa droni ya kijasusi ya Marekani
Rais Donald Trump wa Marekani ametoa radiamali ya kwanza kufuatia kutunguliwa na mfumo wa makombora wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ndege ya kijasusi isiyo na rubani ya Marekani ambapo amedai kwamba, eti Iran imefanya kosa kubwa.
Jana televisheni ya CNN ya Kimarekani ilimnukuu rais huyo wa Marekani katika ujumbe alioutuma kwenye mtandao wa kijamii wa Twitter akidai kwamba, 'Iran imefanya kosa kubwa.' Kwa mujibu wa ripoti hiyo, baada ya Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran (IRGC) kuisambaratisha ndege hiyo ya kisasa ya ujasusi ya Marekani, viongozi wa ngazi ya juu wa serikali ya Trump wamefanya kikao cha dharura katika Ikulu ya White House kujadili suala hilo.
Hata hivyo viongozi hao wa Marekani wamejiepusha kuweka wazi malengo na natija ya kikao hicho, ingawa baadhi ya duru zimeeleza kuhudhuria kikao hicho Patrick M. Shanahan, Kaimu Waziri wa Ulinzi aliyejiuzulu na Mark Esper, naibu wake pia. Hata hivyo Trump hakuwepo katika kikao hicho. Alkhamisi ya jana ndege ya kijasusi ya Marekani aina ya RQ-4 Global Hawk ilitunguliwa na Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu baada ya kuingia katika anga ya Iran katika eneo la Kouh-e-Mobarak katika mkoa wa Hormozgan, kusini mwa nchi. Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na jeshi la IRGC, baada ya ndege hiyo kupaa katika eneo la kusini la Ghuba ya Uajemi na kinyume cha sheria za anga, ilizima alama zake zote za utambulisho wake huku ikiendelea kupaa kutoka upande wa lango la Hormoz kuelekea upande wa mji wa Chabahar. Hatimaye ndege hiyo, baada ya kuingia katika anga ya ardhi ya Iran ilitunguliwa na Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran (IRGC).