Seneti ya Marekani yapinga mauzo ya Trump ya silaha kwa Saudia
Bunge la Seneti la Marekani limeunga mkono azimio la kupinga mauzo ya silaha zenye thamani ya dola bilioni 8.1 kwa Saudi Arabia na Umoja wa Falme za Kiarabu, yaliyoidhinishwa hivi karibuni na utawala wa Rais Donald Trump bila idhini ya Kongresi.
Azimio hilo lilipasishwa katika kikao cha jana Alkhamisi, kwa kura 53 za ndio na 45 za hapana.
Maseneta wa Marekani waliounga mkono azimio hilo la kusimamisha mauzo ya silaha kwa Saudia wakiwemo Lindsey Graham wa chama tawala cha Republican na Bob Menendez wa chama cha upinzani cha Democratic wamesema kupasishwa azimio hilo kwa kuungwa mkono na pande hasimu za kisiasa kunatuma ujumbe wa wazi kwa watawala wa Riyadh.
Wamesema huu sio wakati wa kuwa na miamala ya kawaida ya kibiashara na Saudi Arabia. Nina wasiwasi sana kuhusu historia itakayoachwa nyuma kutokana na mauzo ya silaha hizo.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Mike Pompeo hivi karibuni alisisitiza kuwa, "Mauzo ya silaha kwa Saudia, Imarati na Jordan yakiwemo makombora erevu ya kuelekezwa ya (PGMs) hayawezi kucheleweshwa zaidi, wakati huu ambapo taharuki imeongezeka katika eneo."
Kwa mujibu wa Pompeo, taharuki hiyo katika eneo imeshadidishwa na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Alidai kuwa, "Mauzo ya silaha hizo yatawasaidia waitifaki wetu na kuimarisha uthabiti katika eneo la Asia Magharibi. Silaha hizo zitazisaidia nchi hizo kujilinda dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran."