Jeshi la Marekani latumia helikopta kuwaokoa magaidi wa Daesh Afghanistan
Jeshi la Marekani limetumia helikopta zake kuwaokoa wanachama wa kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh (ISIS) nchini Afghanistan, kufuatia operesheni kali ya wapiganaji wa Taliban ya kulitokomeza genge hilo la ukufurishaji mashariki mwa nchi.
Taarifa ya Taliban imeeleza kuwa, helikopta za kijeshi za US nchini Afghanistan zimewaokoa makamanda na wananachama wa Daesh, waliokuwa kwenye mzingiro kutokana na operesheni ya wiki moja iliyozinduliwa hivi karibuni na wapiganaji wa Taliban, katika mkoa wa Kunar, ulioko mashariki mwa nchi.
Haya yanajiri siku chache baada ya ya ripoti mpya kufichua kuwa, jeshi la Marekani limekuwa likiwaruhusu wanachama wa kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh (ISIS) pamoja na silaha zao kuingia nchini Afghanistan.
Mwaka jana pia, idadi kubwa ya wanachama wa Daesh waliokolewa na jeshi la Marekani kwa kutumia helikopta za kijeshi, baada ya kukabiliwa na kichapo kikali kutoka Taliban katika mkoa wa Jawzjan, kaskazini mwa nchi.
Ripoti iliyochapishwa hivi karibuni na gazeti la Economic Times inabainisha kuwa, jeshi la Marekani limekuwa likiwaruhusu wanachama wa kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh (ISIS) pamoja na silaha zao kuingia nchini Afghanistan.
Katika hali ambayo anga ya Afghanistan ipo chini ya udhibiti wa Marekani na vikosi vya Muungano wa Kijeshi wa Nchi za Magharibi NATO ambavyo viko nchini humo, lakini duru za kuaminika zimeliambia gazeti hilo kuwa, shehena za silaha zimekuwa zikiingizwa nchini humo kwa kutumia helikopta ambazo hazina nembo wala nambari za usajili.
Ripoti hiyo ya gazeti la Economic Times imeeleza kuwa, kwa sasa kuna wanachama zaidi ya 10,000 wa Daesh nchini Afghanistan, na kwamba idadi hiyo inaendelea kuongezeka kila uchao.