Meya wa London amkejeli Trump, asema ni mtoto wa futi sita
https://parstoday.ir/sw/news/world-i54299-meya_wa_london_amkejeli_trump_asema_ni_mtoto_wa_futi_sita
Meya wa jiji la London nchini Uingereza amerudisha mapigo ya mashambulizi ya maneno na bwabwaja za Rais Donald Trump wa Marekani na kumtaja kuwa ni mtoto mdogo mwenye futi 6.
(last modified 2026-03-17T04:36:21+00:00 )
Jun 23, 2019 08:31 UTC
  • Meya wa London amkejeli Trump, asema ni mtoto wa futi sita

Meya wa jiji la London nchini Uingereza amerudisha mapigo ya mashambulizi ya maneno na bwabwaja za Rais Donald Trump wa Marekani na kumtaja kuwa ni mtoto mdogo mwenye futi 6.

Gazeti la The Independent la Uingereza limeripoti kuwa, Meya wa London, Sadiq Khan ambaye alikuwa akihutubia mkusanyiko wa walimu katika jengo la halmashauri ya eneo la la Westminster amesema kuwa simu yake ya kiganjani haipokei jumbe za Twitter za Donald Trump na kumkuejeli Rais wa Marekani kwa kusema: "Wale ambao rununu zao ziko wazi watakapopokea ujumbe wa Twitter kuhusu mimi kutoka kwa mtoto mdogo mwenye futi 6 na nchi 3 katika White House tafadhali wanijulishe."

Wakati wa safari yake mjini London, Rais Donald Trump wa Marekani aliandika ujumbe kwenye mtandao wa kijamii wa Twitter akimfanyia maskhara Meya wa jiji hilo, Sadiq Khan kutokana na ufupi wake. Meya wa London alijibu mapigo akisema: Ujumbe huo ni zaidi ya matusi ya kitoto na haufai kutolewa na Rais wa Marekani.

Donald Trump

Trump alifanya mashambulizi hayo ya ujumbe wa Twitter baada ya Meya wa London kusema kuwa, mienendo ya Rais huyo wa Marekani inafanana na ya mafashisti wa karne ya 20. Vilevile baada ya Sadiq Khan kukosoa mitazamo ya Donald Trump kuhusu Uislamu kiongozi huyo wa Marekani alimtaka Meya wa London akapime kiwango cha akili yake!