Kushadidi makabiliano ya kibiashara baina ya Marekani na Ulaya
Rais Donald Trump wa Marekani kivitendo ameingia katika vita vya kibiashara na akthari ya madola makubwa kiuchumi uulimwenguni.
Hilo limetokana na hatua ya Rais huyo ya kuongeza ushuru kwa bidhaa zinazoingizwa nchini Marekani. Makabiliano haya ya kibiashara hayawahusu washindani wakubwa tu wa Marekani duniani kama China, bali yamewakumba hata washirika wa Washington huko barani Ulaya. Kuhusiana na hilo, ofisi ya Marekani ya uwakilishi wa biashara Jumatatu iliyopita ilipendekeza bei mpya za ushuru zenye thamani ya dola bilioni 4 kwa bidhaa zinazoingizwa nchini humo na huduma kutoka kwa nchi za Umoja wa Ulaya. Bei hizo zimetangazwa kwa mujibu wa orodha ya awali iliyoandaliwa na ofisi hiyo Aprili mwaka huu.
Ushuru huo mpya ni jibu la Marekani kwa ruzuku iliyotolewa na Umoja wa Ulaya kwa sekta ya ndege hususan Airbus na bidhaa zilizoorodheshwa zenye thamani ya dola bilioni 21. Katika hali ambayo Marekani ikitumia kisingizio cha ruzuku hiyo, inataka kuwekwa ushuru mpya dhidi ya bidhaa za Ulaya ilihali yenyewe imetoa ruzuku kubwa katika sekta ya kilimo na kadhalika imekuwa ikipokonya fursa ya ushindani wa mashirika ya Ulaya kama Airbus mkabala na kampuni ya Marekani ya ndege ya Boeing.
Mfano wa wazi wa jambo hili ni kushinda katika hatua ya awali kampuni ya Airbus katika mnada wa kununua ndege maalumu za kujaza mafuta angani kwa ajili ya kikosi cha anga cha Marekani ambapo kwa kuzingatia lobi iliyofanyika, hatimaye mkataba wa mwisho wa biashara hiyo ulitiwa saini na kampuni ya Boeing.
Madola ya Ulaya ambayo kabla ya kipindi cha uongozi wa Rais Donald Trump yalikuwa na uhusiano wa karibu wa kibiashara na Marekani na hata katika kipindi cha uongozi wa Barack Obama kulifanya duru kadhaa za mazungumzo baina ya pande mbili kwa ajili ya kutia saini mkataba wa biashara huru, hivi sasa yanakabiliwa na mazingira na anga tofauti. Rais Donald Trump si tu kwamba, amesimamisha mazungumzo hayo, bali mara kadhaa amechukua hatua za kuziongezea ushuru bidhaa za Ulaya zinazoingia nchini Marekani.
Unyeti wa serikali ya Trump umejikita katika uwanja wa uingizaji magari na vipuri vinaoingia nchini Marekani kutoka Ulaya. Hivi karibuni Trump alitishia kuongeza ushuru mkubwa kwa magari yanayoingia nchini Marekani kutokea Ulaya. Cecilia Malmstrom, Kamishna wa Masuala ya Biashara wa Umoja wa Ulaya amesema katika moja ya hotuba yake kwamba: Endapo Marekani itatekeleza ushuru wa forodha kwa magari ya Ulaya yanayoingizwa nchini humo, jambo hilo litakuwa ni maafa na litaleta mazingira na anga chungu na mbaya.
Tab'an Ulaya nayo imechukua hatua mshabaha kwa ajili ya kukabiliana kibiashara na Washington. Mwanzoni mwa Aprili mwaka huu ilitangazwa kuwa, Umoja wa Ulaya umechukua hatua ya kuandaa orodha ya bidhaa za Marekani kwa ajili ya kukabiliana kibiashara na Washington. Ndege, matrekta, bidhaa za chakula na mikoba ya mkononi ni miongoni mwa bidhaa za Marekani zinazoingizwa Ulaya ambazo zipo katika faharasa ya dola bilioni 20 zinazopaswa kuongezewa ushuru.
Uamuzi huo ni jibu kwa Marekani kufuatia hatua yake ya kuziongezea ushuru bidhaa za Ulaya zinazoingia nchini humo kwa kisingizio cha kupata hasara ya kiuchumi nchi hiyo ya dola bilioni 11 kutokana Ulaya kutoa ruzuku kwa Airbus. Tangu Donald Trump alipoingia madarakani daima amekuwa akiitazama kwa jicho baya biashara huru na kuiona kama sababu kuu ya kulegalega uchumi wa Marekani na kutishia kuondoa vizingiti vilivyoko katika njia hiyo. Hii ni katika hali ambayo, madola ya Ulaya yanaamini kuwa, vita vya kibiashara vimepelekea kupungua na kuzorota mno ukuaji wa uchumi duniani na kwamba, vita hivyo vinaleta hali mpya ya kutokuweko uhakika.
Hasa kwa kutilia maanani kwamba, watakaodhurika zaidi na vita hivi ni watumiaji wa bidhaa kwani bei za bidhaa zitachupa na kupanda. Sasan Shah Weisi, mtaalamu wa masuala ya kiuchumi anasema kuwa, makabiliano ya kibiashara baina ya Ulaya na Marekani yatapelekea kuporomoka uchumi wa pande mbili hizo na hivyo kusababisha kupungua kiwango cha uzalishaji wa kitaifa ulimwenguni.
Utendaji wa Donald Trump unaonyesha kuwa, hata kama atapatiwa upendeleo fulani si tu kwamba, haridhiki na hilo, bali hutaka upendeleo mpya zaidi. Hufanya hilo kupitia mashinikizo na kutumia nyenzo mbalimbali kama kuongeza ushuru wa bidhaa. Kimsingi ni kuwa vita vya kibiashara na kiuchumi ni moja ya vigezo vya wazi vya serikali ya Trump katika utendaji wake. Filihali pia, inaonekana kwamba, serikali ya Trump ambayo mwaka uliopita wa 2018 ilianzisha vita vya muda mfupi vya kibiashara na Ulaya na baada ya hapo kukatekelezwa usitishaji vita baina ya pande mbili, kwa mara nyingine tena imewasha moto wa vita vya biashara kutokana na kuongeza ushuru wa bidhaa.