UN yasikitishwa na hali mbaya inayowakabili wahajiri nchini Marekani
Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa sanjari na kukosoa vikali sera za wahajiri za utawala wa Rais Donald Trump, ameeleza kusikitishwa kwake na hali mbaya inayowakabili wahajiri na wakimbizi nchini Marekani.
Michelle Bachelet alisema hayo jana Jumatatu ambapo alikosoa vikali kitendo cha utawala wa Marekani cha kuwanyimwa mahitaji ya msingi wakimbizi na wahajiri wanaozuiliwa katika vituo vya mpaka wa nchi hiyo.
Hali kadhalika ameitaka serikali ya Marekani ikomeshe sera yake ya kikatili ya kuwatenganisha watoto wadogo na wazazi wao wahajiri katika mpaka wa pamoja wa nchi hiyo na Mexico.
Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa ameeleza bayana kuwa, hatua ya serikali ya Marekani ya kuwatenganisha watoto wa wahajiri na wazazi wao katika mpaka wa Mexico ni ya kikatili na haikubaliki.
Amebainisha kuwa, utekelezaji wa siasa za kuwakamata wahajiri na pia kuwatenga watu wa familia moja, ni kinyume na sheria na misingi ya haki za binadamu na kwamba Marekani inatakiwa kukomesha mwenendo huo mara moja.
Katika hali ambayo Wabunge kadhaa wa Bunge la Wawakilishi nchini Marekani na pia wagombea wa urais katika uchaguzi wa mwaka ujao hivi karibuni walifichua hali mbaya ya afya katika kambi za kuwazuilia wahajiri kwenye mpaka wa nchi hiyo Mexico baada ya kuzitembelea, lakini Rais Donald Trump Jumapili iliyopita alitoa jibu la kejeli na dharau kwa madai hayo.
Alisema, "Kama hali ni mbaya katika vituo vya wahajiri mpakani, basi wahajiri hao waambiwe wasije nchini hapa. Wenyewe wamekimbia umaskini wa kupindukia katika nchi zao."