FBI yatahadharisha, wapinzani wa utawala wa Saudia wako hatarini kuuawa
https://parstoday.ir/sw/news/world-i54741-fbi_yatahadharisha_wapinzani_wa_utawala_wa_saudia_wako_hatarini_kuuawa
Polisi ya Federali nchini Marekani FBI imetahadharisha kwamba, wapinzani wa utawala wa kifalme wa Saudi Arabia na jamaa wa Jamal Khashoggi wanakabiliwa na hatari ya kuuawa.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jul 13, 2019 21:48 UTC
  • FBI yatahadharisha, wapinzani wa utawala wa Saudia wako hatarini kuuawa

Polisi ya Federali nchini Marekani FBI imetahadharisha kwamba, wapinzani wa utawala wa kifalme wa Saudi Arabia na jamaa wa Jamal Khashoggi wanakabiliwa na hatari ya kuuawa.

FBI imewatahadharisha raia wanne wa Saudi Arabia na mpinzani mwingine wa Kiarabu anayeishi Marekani ambaye alikuwa na uhusiano na Jamal Khashoggi, mwandishi habari na mkosoaji wa utawala wa Kifalme wa Saudi Arabia aliyeuawa na maafisa usalama wa Saudia ndani ya ubalozi wa nchi hiyo huko Istanbul nchini Uturuki. kwamba maisha yao yamo hatarini na kwamba huwenda wakauliwa kigaidi na vibaraka wa serikali ya Riyadh. 

Duru za Marekani zinasema kuwa, baada ya mauaji ya Jamal Khashoggi Oktoba mwaka jana, maafisa wa FBI na shirika la ujasusi la Marekani CIA walianzisha mawasiliano na jamaa zake wa karibu walioko Marekani, Canada na Norway kwa sababu mashirika hayo yana wasiwasi kuhusiana na maisha ya watu hao.

CIA: Bin Salman aliamuru mauaji ya Khashoggi

Jamal Khashoggi ambaye alikuwa akikosoa ukiukwaji wa haki za binadamu unaoendelea kufamywa na serikali ya Saudi Arabia na jinai za kivita za nchi hiyo huko Yemen, tarehe Pili Oktoba mwaka 2018 aliuawa kinyama na mwili wake ukakatwa vipande vipande baada tu ya kuingia ndani ya ubalozi wa Saudi Arabia mjini Istanbul. 

Mashirika ya usalama ya Marekani likiwemo shirika la ujasusi la nchi hiyo CIA yamefichua kwamba, mauaji hayo yalifanyika kwa amri ya mrithi wa kiti cha ufalme wa Saudi Arabia, Muhammad bin Salman. Hata hivyo serikali ya Donald Trump inaendelea kumkingia kifua Bin Salman.