Nyaraka: Trump aliiondoa Marekani JCPOA ili kumuudhi Obama
https://parstoday.ir/sw/news/world-i54748-nyaraka_trump_aliiondoa_marekani_jcpoa_ili_kumuudhi_obama
Balozi wa Uingereza mjini Washington aliyejiuzulu siku chache zilizopita baada ya kuhitalifiana na kushambuliana kwa maneno na Donald Trump amesema rais huyo wa Marekani aliiondoa nchi hiyo katika makubaliano ya nyuklia ya JCPOA kwa lengo la kumuudhi mtangulizi wake, Barack Obama.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jul 14, 2019 02:02 UTC
  • Nyaraka: Trump aliiondoa Marekani JCPOA ili kumuudhi Obama

Balozi wa Uingereza mjini Washington aliyejiuzulu siku chache zilizopita baada ya kuhitalifiana na kushambuliana kwa maneno na Donald Trump amesema rais huyo wa Marekani aliiondoa nchi hiyo katika makubaliano ya nyuklia ya JCPOA kwa lengo la kumuudhi mtangulizi wake, Barack Obama.

Katika nyaraka za kumbukumbu zilizovujishwa, Kim Darroch amesema hatua ya Trump ya kuindoa Marekani katika makubaliano ya JCPOA ilichochechewa na chuki zake binafsi dhidi ya Obama na alitaka kulipiza kisiasa na kumghadhabisha mtangulizi wake huyo kwa hatua yake ya kujiondoa JCPOA.

Amesema kitendo hicho cha utawala wa Trump ni sawa na wizi wa kidiplomasia, na Trump hakuwa na sababu za msingi za kuiondoa US kwenye mapatano hayo ya kimataifa.

Balozi huyo wa Uingereza aliyejiuzulu hivi karibuni amebainisha kuwa, "Trump aliondoka JCPOA kwa sababu binafsi kwa kuwa tu iliidhinishwa na rais mstaafu Barack Obama. Kujiondoa kwenye mapatano hayo bila Ikulu ya White House kuwa na chaguo mbadala kuliibua mvutano mkubwa miongoni mwa wapambe wa Trump."

Nchi zilizosalia kwenye JCPOA

Mei mwaka jana na licha ya pingamizi kutoka kwa nchi zilizoidhinisha mapatano hayo ya nyuklia ya mwaka 2015 wakiwemo waitifaki wake, Trump alichukua hatua ya kuiondoa Marekani katika makubaliano hayo.

Trump amekuwa akiyaponda mapatano hayo ya JCPOA hata kabla ya kushinda uchaguzi wa rais nchini Marekani. Kabla ya kuachia ngazi, mwanadiplomasia huyo wa ngazi za juu wa UIngereza mjini Washington alimtaja Trump kama mwanagenzi wa siasa na diplomasia, mtepetevu na asiye na tajriba.