Dunia yamlaani Trump kwa kuwatukana wabunge wanawake wa Marekani
https://parstoday.ir/sw/news/world-i54793-dunia_yamlaani_trump_kwa_kuwatukana_wabunge_wanawake_wa_marekani
Viongozi na wanasiasa kote duniani wameendelea kumlaani Rais Donald Trump wa Marekani kwa kuwadhalilisha na kuwatukana matusi ya kibaguzi wabunge wanawake wa chama cha Democrat katika Kongresi ya Marekani.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jul 16, 2019 02:54 UTC
  • Dunia yamlaani Trump kwa kuwatukana wabunge wanawake wa Marekani

Viongozi na wanasiasa kote duniani wameendelea kumlaani Rais Donald Trump wa Marekani kwa kuwadhalilisha na kuwatukana matusi ya kibaguzi wabunge wanawake wa chama cha Democrat katika Kongresi ya Marekani.

Waziri Mkuu anayeondoka wa Uingereza, Theresa May amesema, "Matamshi ya Trump ya kuwadhalilisha wabunge wanawake wa Kongresi ya nchi hiyo hayakubaliki. Lugha iliyotumika katika ujumbe huo wa Trump haikubaliki."

Naye Jacinda Ardern, Waziri Mkuu wa New Zealand ambaye anasifika kote duniani kwa sera zake za kuwaunga mkono wahajiri na kuwatetea watu wa jamii za walio wachache nchini humo amesema, "Kwa kawaida huwa siingilii siasa za watu wengine, lakini ni wazi kuwa kama walivyofanya watu wengine, na mimi siiungi mkono kauli hiyo ya kibaguzi ya Trump."

Jacinda Ardern, Waziri Mkuu wa New Zealand

Ameongeza kuwa, Bunge la New Zealand limewafungulia mlango watu wa jamii mbalimbali ili kila mmoja ajihisi anawakilishwa, na kwamba mtu hapaswi kuhukumiwa kutokana na asili au chimbuko lake.

Katika ujumbe wake huo, Trump aliandika: "Kwa nini hawarudi na kwenda kusaidia kurekebisha maeneo walikotoka yenye uhalifu? Kisha rudini muje kutuonyesha vipi mumeifanya kazi hiyo. Sehemu hizo zinahitaji sana msaada wenu. Inapasa muondoke haraka iwezekanavyo."

Wabunge wanawake wa Kongresi waliotukanwa na Trump

Wabunge wanawake waliolengwa na Trump kwa matamshi hayo ya chuki za kibaguzi ambao ni Ilhan Omar aliyezaliwa Somalia, Rashida Tlaib mwenye asili ya Palestina, Alexandria Ocasio-Cortez ambaye asili yake ni Puerto Rico na  Ayanna Pressley, Mmarekani mwenye asili ya Kiafrika wamejibu matamshi hayo ya kibaguzi ya Trump na kusema katika taarifa kuwa, "Matamshi ya Trump ni mbinu ya upotoshaji, ili tusiendelee kukosoa utawala wake wa kifisadi, wa kibaguzi na uliofeli."

Wawakilishi hao wa Kongresi ya Marekani wamesema silaha aliyobakia nayo Trump ni ubaguzi tu.

Wakati huohuo, Ibrahim Milhim, msemaji wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina amesema kauli ya Trump ni tusi kwa ofisi ya rais na mfumo wa sheria za Marekani.