Iran: Hatutojadiliana na yeyote kuhusu uwezo wetu wa makombora
Msemaji wa Ofisi ya Uwakilishi ya Iran katika Umoja wa Mataifa amesema Jamhuri ya Kiislamu ya Iran haitafanya mazungumzo na yeyote kuhusu makombora yake ya kujihami.
Alireza Miryousef amesema hayo katika ujumbe alioutuma kwenye mtandao wa kijamii wa Twitter jana Jumanne na kufafanua kuwa, "Tunalishangaa shirika la habari la AP kwa kunukuu vibaya kauli ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Muhammad Javad Zarif katika mahojiano na televisheni ya NBC News, kwamba eti Iran iko tayari kufanya mazungumzo na Marekani kuhusu mradi wake wa makombora. Huo ni upotoshaji wa wazi."
Amesema alichokusudia Dakta Zarif katika mahojiano hayo ni kuwa, "Iwapo Marekani inataka kufanya mazungumzo na Iran kuhusu uwezo wa makombora ya taifa hili, lazima isimamishe uuzaji wa silaha zake yakiwemo makombora katika eneo la Asia Magharibi."
Katika mahojiano hayo na shirika la habari la NBC News, Dakta Zarif alibainisha kuwa, baada ya Marekani kujiondoa katika mapatano ya nyuklia ya JCPOA, kimsingi ilikiuka azimio nambari 2231 la Baraza la Usalama na hivyo haina ustahiki wa kuzungumza kuhusu kukiukwa azimio hilo.
Zarif alisisitiza kuwa azimio hilo haliizuii Iran kufanya majaribio ya makombora yake bali kile inachozuia ni kufanya majaribio ya makombora yanayobeba vichwa vya nyuklia. Ameongeza kuwa Iran haina nia ya kuunda silaha za nyuklia.
Wakati huohuo, Sayyid Abbas Mousavi, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema matamshi ya Dakta Zarif katika mahojiano na NBC News ni sahihi na yasiyokanganya, na kwamba alikusudia kuipa changamoto Marekani iache kurundika silaha katika eneo hili.