Nchi nyingine 8 za Ulaya zajiunga na mfumo wa INSTEX
https://parstoday.ir/sw/news/world-i56352-nchi_nyingine_8_za_ulaya_zajiunga_na_mfumo_wa_instex
Afisa msaidizi wa Mkuu wa Siasa za Nje wa Umoja wa Ulaya amesema nchi 8 zaidi za Ulaya zimejiunga rasmi na mfumo maalumu wa mabadilishano ya fedha kati ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Umoja wa Ulaya (INSTEX).
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Oct 01, 2019 04:29 UTC
  • Nchi nyingine 8 za Ulaya zajiunga na mfumo wa INSTEX

Afisa msaidizi wa Mkuu wa Siasa za Nje wa Umoja wa Ulaya amesema nchi 8 zaidi za Ulaya zimejiunga rasmi na mfumo maalumu wa mabadilishano ya fedha kati ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Umoja wa Ulaya (INSTEX).

Nathalie Tocci, afisa wa karibu wa Federica Mogherini, Mkuu wa Siasa za Nje wa Umoja wa Ulaya alisema hayo jana Jumatatu mjini Sochi nchini Russia na kufafanua kuwa, mbali na nchi waasisi wa mfumo huo, yaani Ujerumani, Ufaransa na Uingereza; nchi nyingine 8 za Ulaya zimejiunga rasmi na mfumo huo.

Hata hivyo hajazitaja nchi hizo za Ulaya zilizojiunga na mfumo wa INSTEX lakini amedokeza kuwa, nchi nyingine mbili za EU zimetangaza azma ya kujiunga na mfumo huo wa kukwepa vikwazo vya Marekani dhidi ya Iran.

Hii ni katika hali ambayo, mwezi Julai mwaka huu, nchi saba yaani Austria, Ubelgiji, Finland, Uholanzi, Slovenia, Uhispania na Sweden zilitoa taarifa ya pamoja zikiunga mkono jitihada zinazotekelezwa ili kufanikisha utendaji kazi wa mfumo huo maalumu.  

Nchi za EU zimetishia kujiondoa JCPOA iwapo Iran itaanza kutekeleza hatua ya nne

Viongozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran mara kadhaa wamekosoa utendaji usioridhisha wa Ulaya katika miezi iliyopita na kutotekelezwa mfumo wa INSTEX; hatua iliyoipelekea Tehran kuchukua pia hatua za kivitendo mkabala wake.

Septemba 6, Tehran ilianza kutekeleza hatua ya tatu ya kupunguza uwajibikaji wake kwa mujibu wa makubaliano hayo ya nyuklia ya JCPOA, na hatua ya nne inatazamiwa kuanza kutekelezwa mwezi ujao wa Novemba.