Nusu ya wapiga kura nchini Marekani hawatampa kura Trump
Uchunguzi wa maoni uliofanywa kwa pamoja na vyombo viwili vya habari vya nchini Marekani unaonyesha kuwa nusu ya wapiga kura nchini humo hawatampigia kura Trump.
Matokeo ya uchunguzi huo wa maoni uliofanywa na televisheni ya NBC na gazeti la Wall Street Journal yanaonyesha kuwa Rais wa Marekani ana kibarua kigumu ili kushinda uchaguzi wa mwaka ujao wa 2020.
Televisheni ya NBC jana usiku ilitangaza kuwa matokeo ya uchunguzi huo wa maoni yanaonyesha kuwa karibu nusu ya wapiga kura waliojiandikisha wameamua kuwa hawatampigia kura Donald Trump bila ya kujali mgombea wa kiti cha urais wa chama cha Democrat atakuwa nani.
Kwa mujibu wa matokeo hayo ya uchunguzi wa maoni; asilimia 46 ya washiriki wamesema kuwa hakuna shaka kwamba watampigia kura mgombea ambaye si Trump; na ni asilimia 34 tu ya washiriki wa uchunguzi huo wa maoni waliosema kuwa watampigia kura Trump.
Aidha asilimia 17 ya washiriki wamesema kuwa kupiga kwao kura kutategemea ni mgombea yupi wa kiti cha rais atakiwakilisha chama cha Democrat katika uchaguzi huo wa mwakani. Siasa za Rais Donald Trump ndani ya Marekani na hata baina yake na waitifaki wa Ulaya wa White House zimekosolewa pakubwa ndani ya nchi hiyo na kimataifa.