Madai ya Trump: 'Sina hofu ya kusailiwa'
Rais Donald Trump wa Marekani amedai kwamba hana hofu yoyote na mwenendo wa kusailiwa kwake.
Rais huyo wa Marekani anayeandamwa na kashfa mbalimbali amesema kuwa, hahofii kusailiwa kwa kuwa hajawahi kuwadhuru watu wanaotazamiwa kutoa ushahidi dhidi yake. Aidha ameongeza kwamba hakuna mtu mwenye taarifa muhimu. Akiendelea kubainisha suala hilo, Trump amedai kwamba Warepublican wamechukizwa na hatua ya Wademocrat kuhusiana na suala la kusailiwa kwake. Madai ya rais huyo wa Marekani kwamba hana wasi wasi wowote kuhusiana na suala la kusailiwa, ameyatoa katika hali ambayo ripoti zinaonyesha kwamba amekuwa akiwazuia baadhi ya maafisa wa Ikulu ya White House kutoa ushahidi mbele ya kongresi ya nchi hiyo.
Katika mawasiliano ya simu kati yake na Rais Volodymyr Zelensky wa Ukraine hapo mwezi Julai mwaka huu, yaliyokuja kufahamika kwa jina la 'Ukrainegate', Trump alimtaka rais huyo kumpatia taarifa za Hunter Biden, mtoto wa kiume wa Joe Biden, mshindani wake tarajiwa wa chama cha Democrat katika uchaguzi wa mwakani. Kufuatia hali hiyo Wademocrat walianzisha mchakato wa kumsaili rais huyo, ambao bado unaendelea.