Trump, changamoto kubwa zaidi kwa Umoja wa Ulaya
https://parstoday.ir/sw/news/world-i57582-trump_changamoto_kubwa_zaidi_kwa_umoja_wa_ulaya
Tokea aingie madarakani mwezi Januari 2017, Rais Donald Trump wa Marekani amekuwa akitekeleza siasa za upande mmoja na kuiondoa nchi hiyo katika mitakaba muhimu ya kimataifa, kinyume kabisa na matarajio na mitazamo ya Umoja wa Ulaya na hivyo kupanua pengo la tofauti kati ya pande hizo mbili za Bahari ya Atlantiki.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Nov 30, 2019 01:01 UTC
  • Trump, changamoto kubwa zaidi kwa Umoja wa Ulaya

Tokea aingie madarakani mwezi Januari 2017, Rais Donald Trump wa Marekani amekuwa akitekeleza siasa za upande mmoja na kuiondoa nchi hiyo katika mitakaba muhimu ya kimataifa, kinyume kabisa na matarajio na mitazamo ya Umoja wa Ulaya na hivyo kupanua pengo la tofauti kati ya pande hizo mbili za Bahari ya Atlantiki.

Ni kutokana na jambo hilo ndipo nchi za Ulaya zikawa zinakosoa sana siasa hizo za Trump. Katika msimamo wake wa hivi karibuni kabisa kuhusu siasa hizo za upande mmoja za Marekani, Donald Tusk, Rais wa Baraza la Umoja wa Ulaya amesema kuwa Rais Donald Trump wa Marekani ndiye chongamoto kubwa zaidi kwa umoja huo, kwa kuwa hivi sasa anaomba dua ya Uingereza kutengana na Umoja wa Ulaya. Trump amepokea vizuri uamuzi wa Uingereza kujiondoa katika Umoja wa Ulaya na kuitaja Ulaya kuwa adui wake wa kibiashara ambaye pia anatilia shaka thamani za shirika la kujihami, Nato. Tusk amesema: Ni mara ya kwanza katika historia ambapo rais wa Marekani anaupinga wazi wazi Umoja wa Ulaya. Anaunga mkono Brexit na kuomba dua kwa ajili ya Uingereza itengane na Umoja wa Ulaya. Tusk pia amesema kuwa Trump anataka kuudhoofisha Umoja wa Ulaya na kusisitiza kuwa huenda jambo hilo likawa changamoto kubwa zaidi kwa umoja huo. Uhusiano wa Marekani na Umoja wa Ulaya umekuwa ukipitai hali ngumu tokea Trump aingie madarakani White House, hata kama hivi karibuni, yaani mwezi Septemba mwaka huu, Mike Pompeo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani alisafiri mjini Brussels kwa madhumuni ya kujaribu kuimarisha uhusiano wa pande mbili.

Trump ambeye anatekeleza kwa nguvu zake zote siasa za upande mmoja duniani

Brussels na Washington zinatofautiana kuhusiana na mambo mengi ya kisiasa, kibiashara, kijeshi, kiusalama na hali ya hewa. Uamuzi wa Trump wa kuiondoa Marekani katika mikataba muhimu ya kimataifa ikiwemo ya JCPOA, wa Tabianchi wa Paris, Makombora ya Wastani ya Nyuklia, kusimamishwa kwa mapatano ya biashara huru kati ya pande mbili za Bahari ya Atlantiki na pia kuwepo mivutano ya kibiashara na Umoja wa Ulaya ni mambo ambayo yamewakasirisha sana viongozi wa umoja huo na wa bara Ulaya kwa ujumla. Kinyume na Barack Obama, rais wa zamani wa Marekani ambaye alikuwa muungaji mkono mkubwa wa Uingereza kuendelea kubakia katika Umoja wa Ulaya, Trump amekuwa akimchochea Boris Johnson, Waziri Mkuu wa Uingereza aitoe nchi hiyo katika umoja huo hata bila ya kufikiwa mapatano ya mwisho na umoja huo kuhusiana na masuala muhimu ya pande mbili. Uchochezi huo umewakasirisha sana viongozi wa ngazi za juu wa Umoja wa Ulaya akiwemo Donald Tusk, Rais wa Baraza la umoja huo. Kwa mtazamo wa Ulaya, lengo kuu la Trump kuitaka Uingereza ijitoa haraka katika umoja huo, ni kuanzisha uhusiano mkubwa wa kiuchumoi na serikali ya London ili kujinufaisha zaidi na soko na fursa nzuri za kibiashara za nchi hiyo ya Ulaya. Kwa mujibu wa Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa, kujitoa Uingereza katika Umoja wa Ulaya bila kufikiwa mapatano, kunaweza kuifanya nchi hiyo kuwa mshirika mkubwa wa Marekani na serikali iliyo chini ya udhibiti wa Washington.

Donald Tusk, Rais wa Baraza la Umoja wa Ulaya

Rais wa Marekani anaamini kwamba kwa miongo kadhaa sasa, Ulaya imekuwa ikiitumia vibaya nchi hiyo kwa lengo la kujidhamini maslahi ya kiuchuni na kwamba sasa wakati umefika kwa Marekani kubadilisha mkondo wa mambo kwa maslahi yake. Trump anakosoa vikali siasa za nchi za Ulaya kutetea upande wake na kusema: Hata kama Umoja wa Ulaya unaonekana kidhahiri kuwa ni mzuri na wa kuvutia lakini hauna huruma na kimsingi ulibuniwa kwa ajili ya kutunyanyasa.

Kwa msingi huo, serikali ya Trump inataka kubadilisha uhusiano wa kibiashara na kiuchumi uliopo kati ya Marekani na Ulaya na hasa kuhusiana na suala la kuarifishiwa ushuru mpya bidhaa za Ulaya zinazoingizwa nchini Marekani, jambo ambalo limeamsha hasira ya nchi za bara hilo na kuzipelekea kutishia kutazama upya viwango vya ushuru wa bidhaa za Marekani zinazoingizwa katika nchi hizo. Kupitia nara yake ya 'Marekani Kwanza', Trump amekuwa akiyaweka mbele maslahi ya Marekani bila kujali ya upande wa pili, na hata ya washirika wake wa karibu sana wa Ulaya, na kudhani kwamba siasa zake za upande mmoja na za kujijali peke yake, zitaongeza nguvu ya nchi hiyo dhidi ya washindani wake. Pamoja na hayo lakini  matokeo ya siasa hizo tokea aingie madarakani nchini Marekani yanathibitisha wazi kwamba hazijamsaidia  na lolote bali zimekuwa zikiipelekea Marekani kutengwa zaidi duniani.