Iran na Russia zaonya kuhusu kuhamishiwa magaidi wa Daesh Afghanistan
https://parstoday.ir/sw/news/world-i57966-iran_na_russia_zaonya_kuhusu_kuhamishiwa_magaidi_wa_daesh_afghanistan
Maafisa wa ngazi za juu wa usalama wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Russia wameonya kuhusu njama za makusudi za kuwahamishia wanachama wa kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh nchini Afghanistan.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Dec 18, 2019 23:02 UTC
  • Iran na Russia zaonya kuhusu kuhamishiwa magaidi wa Daesh Afghanistan

Maafisa wa ngazi za juu wa usalama wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Russia wameonya kuhusu njama za makusudi za kuwahamishia wanachama wa kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh nchini Afghanistan.

Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Iran na Nikolai Patrushev, Katibu wa Baraza la Usalama la Serikali ya Kifederali ya Russia walisema hayo jana Jumatano pambizoni mwa Duru ya Pili ya Mkutano wa Usalama wa Eneo hapa jijini Tehran na kusisitiza kuwa, mabaki ya kundi la kigaidi la Daesh (ISIS) yamehamishiwa Afghanistan kutoka Syria na Iraq.

Shamkhani ameeleza bayana kuwa, "Tangu kundi la Daesh lishindwe katika nchi za Syria na Iraq, changamoto kuu ya kiusalama katika eneo ni kusambazwa wanachama wa genge hilo nchini Afghanistan. Lengo kuu la kutaka kulihuisha na kuliratibu upya kundi hilo ni kutaka litekeleze mashambulizi ya kigaidi katika nchi hiyo ya Asia ya Kati na jirani zake."

Ameongeza kuwa, uwepo wa majeshi ya nchi ajinabi katika eneo hili, umechochea taharuki na ukosefu wa usalama. Wakati huohuo, Shamkhani amepongeza sera na msimamo wa Moscow wa kupinga hatua ya Marekani ya kujiondoa kwenye makubaliano ya nyuklia ya JCPOA, na kusisitiza kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran itaendelea kuchukua hatua za kupunguza uwajibikaji wake kwenye mapatano hayo. 

Baadhi ya washiriki wa mkutano wa usalama jijini Tehran

Kwa upande wake, Nikolai Patrushev, Katibu wa Baraza la Usalama la Serikali ya Kifederali ya Russia amesema Marekani ndiyo inayowahamishia wanachama wa Daesh nchini Afghanistan. Amesema hivi sasa kuna wanachama kati ya 2,500 na 4,000 wa genge hilo la ukufurishaji nchini Afghanistan.

Mbali na Iran na Russia, maafisa wengine wa ngazi za juu wa usalama wa Russia, China, India, Afghanistan, Tajikistan, na Uzbekistan wameshiriki mkutano huo wa usalama wa siku moja hapa jijini Tehran.