Ripoti: Marekani ni kituo kikubwa zaidi duniani cha kuhifadhi fedha 'chafu'
Ripoti mpya ya shirika la Tax Justice Network (TJN) imeituhumu Marekani kuwa ndicho kitovu kikubwa zaidi duniani cha kuficha na kutakatisha fedha haramu.
Katika ripoti yake ya mwaka huu 2020, shirika hilo limesema sheria mbovu za fedha zinaifanya Marekani iwe nchi yenye usiri mkubwa zaidi duniani katika kuhifadhi na kutakatisha fedha haramu.
Ripoti hiyo imesema usiri huo wa kuhifadhi fedha chafu nchini Marekani umeongezeka kwa asilimia 15 na kulifanya taifa hilo la kibeberu liipiku Uswisi, na kuwa la kwanza duniani kwa ufisadi huo wa kifedha. Imarati, Uholanzi, Singapore na Uswisi ni katika nchi 10 zinazoongoza kwa uozo huo wenye taathira hasi kwa chumi za nchi mbalimbali duniani.
Haya yanajiri katika hali ambayo, mwanamke tajiri zaidi barani Afrika anatuhumiwa kutumia mashirika ya fedha ya Marekani kuhifadhi, kutakatisha na kuhamisha fedha zake kinyume cha sheria.
Hivi karibuni, vyombo kadhaa vya habari vya ndani na nje ya Angola vilichapisha mamia ya maelfu ya nyaraka zilizofichuliwa na Jumuiya ya Kimataifa ya Wanahabari Wapekuzi (ICIJ) kuhusu namna Isabel dos Santos, mfanyabiashara bilionea na binti wa rais wa zamani wa nchi hiyo, Jose Eduardo dos Santos, alivyofyonza utajiri wa nchi hiyo, wakati babake akiwa rais.
Isabel dos Santos aliye na umri wa miaka 46 na ambaye sehemu kubwa ya utajiri wake ipo Marekani na katika nchi za Ulaya na Imarati, amekuwa akikanusha tuhuma dhidi yake akisema hazina msingi wowote. Bilionea huyo alihama Angola baada ya baba yake, Jose Eduardo dos Santos aliyetawala nchi hiyo kwa karibu miaka 40, kuondoka madarakani mwaka 2017 na nafasi yake kuchukuliwa na Joao Lourenco.