Iran kuendelea kushirikiana na IAEA katika uga wa nyuklia
https://parstoday.ir/sw/news/world-i59532-iran_kuendelea_kushirikiana_na_iaea_katika_uga_wa_nyuklia
Balozi na Mwakilishi wa Kudumu wa Iran katika mashirika ya kimataifa mjini Vienna, Austria amesema Iran itaendelea kushirikiana na Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA) kuhusu utekelezwaji wa mapatano ya nyuklia ya Iran yanayojulikana kama Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezaji (JCPOA).
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Mar 04, 2020 01:05 UTC
  • Iran kuendelea kushirikiana na IAEA katika uga wa nyuklia

Balozi na Mwakilishi wa Kudumu wa Iran katika mashirika ya kimataifa mjini Vienna, Austria amesema Iran itaendelea kushirikiana na Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA) kuhusu utekelezwaji wa mapatano ya nyuklia ya Iran yanayojulikana kama Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezaji (JCPOA).

Akizungumza na waandishi habari Jumanne, Kazem Gharibabadi ameashiria kutolewa ripoti mpya ya IAEA kuhusu namna Iran inavyotekeleza mapatano ya JCPOA na kusema IAEA imekuwa ikichunguza namna Iran inavyotekeleza mapatano hayo tokea Januari 16 mwaka 2016.

Gharibabadi amesema ripoti hiyo mpya ya IAEA  imesema hadi kufikia Februari 19 mwaka huu, Iran ilikuwa imerutubisha kilo 1020.9 za madini ya urani.

Gharibabadi amesema Iran inaendelea kujitolea kutekeleza kwa muda Protokali Ziada ya nyuklia. 

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ilianzia kupunguza hatua kwa hatua uwajibikaji wake ndani ya makubaliano ya JCPOA mwezi Mei mwaka uliopita mwaka mmoja baada ya Marekani na pande za Ulaya kuacha kutekeleza majukumu yao ndani ya makubaliano hayo ya nyuklia. 

Vipengee nambari 26 na 36 vya makubaliano ya JCPOA vinaeleza kuwa, Iran inayo haki ya kusimamisha kikamilifu kwa upande mmoja uwajibikaji wake ndani ya makubaliano hayo iwapo upande wa pili nao hautatekeleza majukumu yake.