Kongresi: Wamarekani milioni 150 huenda wakaambukizwa Corona
Bunge la Marekani (Kongresi) limesema inakisiwa kuwa Wamarekani kati ya milioni 70 hadi 150 watakumbwa na virusi vya Corona ambavyo vimeua maelfu ya watu katika maeneo mbalimbali duniani.
Mbunge wa Kongresi, Rashida Tlaib alitoa makadirio hayo jana Alkhamisi katika kikao cha Bunge la Wawakilishi la Marekani na wanachama wa jopokazi la kupambana na Corona la Ikulu ya White House, na hivyo kuthibitisha takwimu za kukisia zilizokuwa zimetolewa huko nyuma na vyombo vya habari vya nchi hiyo kama NBC News na Axios.
Kufikia jana Alkhamisi, kesi 1,300 za Corona zilikuwa zimenakiliwa nchini Marekani, huku virusi hivyo vikiua Wamarekani 38.
Katika hatua nyingine, imebainika kuwa, Waziri wa Mambo ya Ndani wa Australia ambaye alikutana na binti ya Rais Donald Trump, Ivanka Trump siku chache zilizopita, amethibitishwa kuwa na virusi hivyo.
Peter Dutton ambaye alikutana na Ivanka mnamo Machi 6, pamoja na Mwanasheria Mkuu wa Marekani, William Barr, jijini Washington amewekwa karantini hospitalini kuanzia leo Ijumaa baada ya kuthibiti kuwa ameambukizwa virusi hivyo.
Hivi sasa wananchi wa Marekani wanamshutumu vikali rais wa nchi hiyo Donald Trump kwa kudharau wimbi hilo la maambukizi ya virusi vya Corona nchini humo, kiasi cha kudai kuwa ataendelea kufanya kampeni zake za kisiasa, mbali na kukataa kupimwa ugonjwa huo licha ya kukutana na afisa wa Bazil mwenye Corona.