Hofu ya Corona; Wamarekani wapiga foleni kununua bunduki
https://parstoday.ir/sw/news/world-i59791-hofu_ya_corona_wamarekani_wapiga_foleni_kununua_bunduki
Foleni ndefu zimeonekana nje ya maduka ya kuuza bunduki na silaha za moto nchini Marekani, wakati huu ambapo wananchi wa nchi hiyo wananunua bidhaa muhimu za msingi kwa pupa kutokana na hofu ya ugonjwa wa Corona.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Mar 17, 2020 04:24 UTC
  • Hofu ya Corona; Wamarekani wapiga foleni kununua bunduki

Foleni ndefu zimeonekana nje ya maduka ya kuuza bunduki na silaha za moto nchini Marekani, wakati huu ambapo wananchi wa nchi hiyo wananunua bidhaa muhimu za msingi kwa pupa kutokana na hofu ya ugonjwa wa Corona.

Duru za habari zinaarifu kuwa, mauzo ya silaha za moto nchini humo hususan katika jimbo la California yameongezeka kwa kiasi kikubwa huku taifa hilo likiendelea kurekodi maambukizi zaidi ya Corona (Covid-19).

Mmoja wa wauzaji wa maduka ya bunduki mjini Charlotte eneo la Carolina Kaskazini akizungumzia foleni hizo ndefu za wananchi wa Marekani kununua bunduki, ameliambia gazeti la The Guardian kuwa, "hii ni mara yangu ya pili katika miaka 61 ya kufanya biashara hii, kuona taswira ya namna hii."

Karibu majimbo yote 50 ya Marekani yamekumbwa na maradhi hayo hatarishi, ingawaje serikali ya Washington inasema waliombukizwa virusi hivyo ni watu 3,487, huku 68 wakipoteza maisha.

Duka la kuuza silaha za moto nchini Marekani

Anthony Fawcie, Mkuu wa Taasisi ya Kitaifa ya Kudhibiti Maradhi ya Kuambukiza nchini Marekani ametahadharisha juu ya ongezeko la vifo vinavyotokana na virusi vya Corona kufikia malaki ya watu, na kusema kuwa iwapo hatua za lazima hazitochukuliwa, hali itakuwa mbaya sana.

Maafisa wa afya na wataalamu wa miripuko ya magonjwa wa Kituo cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa Marekani (CDC) wanakadiria kuwa, yumkini ugonjwa wa Corona ukaua Wamarekani milioni moja na laki saba, mbali na milioni 160 hadi 214 kuambukizwa.