Kituo cha Kiislamu chachomwa moto Marekani siku ya kwanza ya Ramadhani
https://parstoday.ir/sw/news/world-i60609-kituo_cha_kiislamu_chachomwa_moto_marekani_siku_ya_kwanza_ya_ramadhani
Baraza la Uhusiano wa Kiislamu nchini Marekani (CAIR) limezitaka mamlaka husika nchini humo kuchunguza kitendo cha kuteketezwa kwa moto Kituo cha Kiislamu katika jimbo la Missouri, katika siku ya kwanza ya mwezi mtukufu wa Ramadhani.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Apr 26, 2020 07:55 UTC
  • Kituo cha Kiislamu chachomwa moto Marekani siku ya kwanza ya Ramadhani

Baraza la Uhusiano wa Kiislamu nchini Marekani (CAIR) limezitaka mamlaka husika nchini humo kuchunguza kitendo cha kuteketezwa kwa moto Kituo cha Kiislamu katika jimbo la Missouri, katika siku ya kwanza ya mwezi mtukufu wa Ramadhani.

Ibrahim Hooper, Mkuu wa Ofisi ya Mawasiliano ya baraza hilo sambamba na kulaani jinai hiyo amesema, "tunaziomba mamlaka husika kuanzisha uchunguzi ili kubainia kiini cha moto huo, kwa kuwa umetokea kwenye nyumba ya ibada na katika kipindi muhimu cha kidini."

Amesema wana mashaka na moto huo ulioteketeza jengo la Kituo cha Kiislamu cha Cape Girardeau, yapata kilomita 185 kusini mwa St Louis, jimboni Missouri, kwa kuwa umejiri katika kipindi muhimu sana kwenye kalenda ya waumini wa Kiislamu.

Baraza la Uhusiano wa Kiislamu nchini Marekani limesema msikiti ulioko kwenye jengo hilo umeharibiwa vibaya kutokana na moto huo, pamoja na sehemu ya kuingia hadi ghorofa ya pili ya jengo hilo.

Mkuu wa Idara ya Zimamoto katika jimbo hilo, Travis Hollis amesema watu 15 walinusurika kifo kwenye moto huo, na kuongeza kuwa jengo hilo limeteketea vibaya. 

Wamarekani wenye chuki dhidi ya Uislamu na Waislamu

Hivi karibuni, Baraza la Uhusiano wa Kiislamu nchini Marekani (CAIR) lilionya kuwa vitendo vya uhalifu vinavyotokana na chuki dhidi ya Waislamu vimeongezeka nchini humo kwa kiwango cha kutisha. Chuki dhidi ya Uislamu na Waislamu na mashambulio dhidi ya Waislamu na wahajiri yameongezeka mno nchini Marekani tangu baada ya kuingia madarakani Donald Trump mwaka 2017. 

Februari mwaka huu, Antonio Guterres, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa alisema kuwa anatiwa wasiwasi na kuongezeka vitendo vya chuki dhidi ya Uislamu duniani na akasema mwenendo huo hauvumiliki na unapaswa kukabiliwa kwa nguvu zote.