Rais Erdoğan asisitiza kuwa Uturuki ni rafiki wa kuaminika wa Marekani
Rais Recep Tayyip Erdoğan wa Uturuki amemuandikia barua Rais Donald Trump wa Marekani akikariri kuwa Ankara ni mshirika wa kuaminika wa Washington, huku akisisitiza juu ya mshikamano wa pande mbili.
Rais Erdoğan ameyasema hayo katika barua aliyoituma Marekani siku ya Jumanne pamoja na misaada ya kiafya na kitiba ya Uturuki kwa nchi hiyo ambapo katika barua hiyo amesema kuwa, Washington inatakiwa iwe na uhakika kwamba Uturuki ni mshirika wa kuaminika na wa daima wa Marekani katika eneo. Katika barua hiyo pia rais wa Uturuki amesisitiza kuwa, matukio ya hivi karibuni katika eneo yameonyesha kwamba kuendelea umoja na ushirikiano imara kati ya Marekani na Uturuki, ni suala lenye umuhimu mkubwa.
Sisitizo la Rais Erdoğan juu ya mshikamano wa Washington na Ankara, limetolewa katika hali ambayo kwa mara kadhaa serikali ya Uturuki imekuwa ikiituhumu Washington kwa kuwaunga mkono wapiganaji wa Kikurdi wa PKK wanaopigana dhidi ya serikali ya Ankara, suala ambalo daima limekuwa likitia doa uhusiano wa pande mbili hizo. Mbali na hayo kwa mara kadhaa Marekani imetishia kuiwekea vikwazo serikali ya Uturuki kutokana na uamuzi wake wa kununua ngao ya makombora ya S-400 kutoka Russia.