Jun 05, 2020 05:57 UTC
  • Malalamiko ya UN dhidi ya ubaguzi wa rangi wa kitaasisi nchini Marekani

Ubaguzi wa rangi na kizazi na ukandamizaji uliochupa mipaka dhidi ya watu wasio wazungu hasa wenye asili ya Afrika huko Marekani una historia ndefu na ulianza tangu ilipoasisiwa nchi hiyo karne tatu zilizopita. Ubaguzi huo daima umekuwa ni sifa inayochukiza ya jamii ya Marekani. Licha ya Wamarekani wenye asili ya Afrika kuendesha mapambano makali ya kupigania haki zao, lakini hadi leo hii wanaendelea kuwa wahanga wa ubaguzi, ukatili na ukandamizaji usio na kifani.

Hali hiyo mbaya imeufanya Umoja wa Mataifa ambacho ndicho chombo kikubwa zaidi cha kimataifa dauniani, kuilalamikia na kuikosoa Marekani kwa ubaguzi na unyanyasaji wake huo wa kitaasisi na kiserikali. Michelle Bachelet, Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa amekosoa ubaguzi wa jadi huko Marekani na ameelezea kusikitishwa pia na jinsi waandishi wa habari wanavyoshambuliwa vibaya huko Marekani wakati wanaporipoti machafuko na ukatili unaoendelea nchini humo. Katika tamko lake, Bachelet amesema: Sauti zinazopigania kukomeshwa mauaji ya Wamarekani Waafrika wasio na silaha inabidi ziachiwe zisikike. Vile vile sauti zinazopigania kukomeshwa ukandamizaji wa polisi na sauti zinazopigania kukomeshwa ubaguzi wa kitaasisi na ulioenea katika jamii ya Marekani lazima ziachiwe zisikike.

Michelle Bachelet, Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa

 

Matamshi hayo yametolewa katika hali ambayo malalamiko makubwa ya maelfu ya watu wanaoshiriki kwenye maandamano ya kila siku katika majimbo tofauti ya Marekani kulaani ubaguzi wa rangi na ukandamizaji wa jeshi la polisi la nchi hiyo dhidi ya Wamarekani wenye asili ya Afrika hasa baada ya Mmarekani mwenye asili ya Afrika anayejulikana kwa jina la George Floyd kuuliwa kinyama na kikatili na Mmarekani mzungu huko Minneapolis, bado yanaendelea kwa nguvu zote.

Licha ya kwamba karibu asilimia 13 ya jamii ya Marekani inaundwa na Wamarekani wenye asili ya Afrika, lakini hawapewi fursa ya kufaidika na utajiri wa nchi, elimu na ustawi wa kijamii. Lakini tukija katika masuala hasi kama vile idadi kubwa ya wafungwa katika jela za Marekani, waathiriwa wengi wa magonjwa mbalimbali, unyanyasaji na ubaguzi, tutaona kuwa asilimia ya Wamarekani wenye sili ya Afrika ndiyo kubwa kupindukia ikilinganishwa na wazungu. Ubaguzi wa rangi na wa kizazi daima imekuwa ndiyo sifa mbaya ndani ya jamii ya Marekani katika historia yote ya karne tatu ya tangu kuasisiwa nchi hiyo. Wimbi kubwa la utumwa, kutumiwa vibaya Waafrika, kuuliwa kama wanyama, kuteswa na kunyanyaswa kupindukia, kunajisiwa na kutumiwa vibaya kijinsia, kunyanyapaliwa na madhila mengineyo mengi ni katika sifa mbaya ambazo zimekuwepo katika jamii ya Marekani miaka yote hii na hiyo ni sehemu ndogo tu ya mateso mengi wanayofanyiwa Wamarekani wenye asili ya Afrika muda wote huo. Ijapokuwa katika muongo wa 1950 sheria za Marekani zilibadilishwa na likaanza wimbi fulani la kutambuliwa haki za Waafrika na kuondolewa manyanyaso, lakini jamii iliyooza kwa ubaguzi ya Marekani hadi leo hii inaendeleza unyanyasaji na ubaguzi ule ule uliokuwepo dhidi ya watu wasio wazungu tangu ilipoundwa nchi ya Marekani.

Machafuko nchini Marekani

 

Hali ya Wamarekani Waafrika ni mbaya sana pia kiuchumi, kijamii, kiusalama, kiafya n.k. Moja ya mambo yanayodhihirisha wazi jambo hilo katika miaka ya hivi karibuni ni kuongezeka ukandamizaji wa jeshi la polisi dhidi ya Wamarekani hao. Wahanga wakuu wa ukandamizaji wa polisi nchini Marekani ni watu wasio wazungu na hasa Waafrika na hiyo ndiyo sababu kuu ya kushuhudiwa maandamano na uasi unaotokea mara kwa mara katika miji mbalimbali ya Marekani. 

Kiujumla ni kwamba hali ni mbaya nchini Marekani. Ubaguzi wa kuchupa mipaka, uzembe wa viongozi hasa katika janga kama la corona, jinai za kiuchumi na kijeshi za Marekani nje ya nchi hiyo dhidi ya nchi ambazo hata hazijawahi kuishambulia Marekani, matatizo ya kiuchumi na ukosefu wa kazi, yote hayo yamewafanya Wamarekani katika kila kona ya nchi hiyo wamiminike mabarabarani na kaulimbi mbio inayosema: "Tumechoka, tuacheni tupumue." Lakini pia hali hiyo inalalamikiwa na kukosolewa kimataifa malalamiko hayakuishia ndani ya Marekani tu. Michelle Bachelet, Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa pamoja na mambo mengine amesema: ...hasa wakati wa mgogoro, viongozi wa nchi husika wanapaswa kulaani waziwazi ubaguzi wa rangi; watafakari ni kitu gani kimewachemsha na kuwakasirisha wananchi; wawasilikize, wapate funzo na wachukue hatua ambazo kwa hakika zitaondoa dhulma na ukosefu wa uadilifu. Kama Marekani ina nia kweli ya kusonga mbele, basi haina budi kusikiliza malalamiko yanayohusiana na maandamano ya upinzani yanayoendelea hivi sasa katika mamia ya miji ya Marekani na kuyatekeleza kivitendo. 

Hata Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa nalo limewataka viongozi wa Marekani kuchukua hatua za kivitendo za kukomesha ubaguzi wa rangi na ukandamizaji dhidi ya Wamarekani wasio wazungu hususan Waafrika na limeonya vikali kuhusu madhara ya kutosikilizwa vilio na malalamiko ya haki ya wananchi wa Marekani.

Tags