Amri mpya ya Trump yaidhinisha kuendelea ukatili wa polisi ya Marekani
Ukatili na utumiaji mabavu usio na mipaka wa polisi ya Marekani dhidi ya watu wenye asili ya Afrika ambao unatekelezwa katika sera jumla ya ubaguzi wa rangi umeubia maandamano ambayo hayajawahi kushuhudiwa Marekani. Hali hiyo imempelekea rais mwenye utata wa nchi hiyo, Donald Trump, kutoa amri mpya ya kile alichodai kuwa ni mabadiliko katika muundo wa polisi nchini humo.
Siku ya Jumanne, Trump alitia saini dikrii ya kutekelezwa kile kinachotajwa kuwa ni mabadiliko katika muundo wa polisi. Trump amechukua hatua hiyo baada ya zaidi ya wiki tatu za maandamano ya kihistoria Marekani yaliyoanza baada ya polisi mzungu kumuua kinyama George Floyd, Mmarekani mwenye asili ya Afrika. Mnamo Mei 25, afisa wa polisi katika mji wa Minneapolis jimboni Minnesota nchini Marekani alimbinya shingo kwa kutumia goti kwa muda dakika 9 hivi George Floyd, hadi akakata roho. Katika amri yake hiyo Trump ametangaza kuwa 'mbinu ya kubinya shingo' ni kinyume cha sheria lakini wakati huo huo akasema maafisa wa polisi wanaruhusiwa kutumia mbinu hiyo iwapo maisha yao yatakuwa hatarini. Akizungumza katika Ikulu ya White House amesema dikrii hiyo imetaka mbinu ya kubinya shingo ipigwe marufuku isipokuwa tu wakati maisha ya polisi yako hatarini.
Dikrii hiyo ya Trump itapelekea kuanzishwa mtandao ambao utakuwa na taarifa za maafisa wa polisi ambao wana rekodi ya kutumia mabavu ili wafuatiliwe. Katika hotuba yake, Trump hakuashiria hata kidogo 'ubaguzi wa rangi ulioratibiwa' ambao umekita mizizi katika Idara ya Polisi ya Marekani.
Trump amesema bila kuwepo na polisi jamii itakumbwa na ukosefu wa usalama na hali ya uvunjaji sheria na kwa kisingizio hicho amekataa kuamurusha uchunguzi wa kina kuhusu vitendo vya ukatili na utumiaji mabavu katika idara ya polisi na njia za kuhitimisha tatizo hilo. Trump amejaribu kuonyesha kuwa maandamano ya sasa ya wanaopinga ubaguzi ni maandamano ya kupinga uwepo wa polisi na hivyo amesisitiza kuhusu ulazima wa kudumishwa jeshi la polisi.
Dikrii hiyo ya Trump imekosolewa vikali kutokana na udhaifu wake mkubwa. Wakosoaji wanasema dikrii hiyo haina mabadiliko ya kimsingi na ya lazima yanayohitajika kuzuia hatua za mabavu na ukatili katika jeshi la polisi nchini humo. Wanasiasia wa chama cha upinzani cha Democrats na makundi mengine ya watetezi wa haki wamekosoa vikali dikrii hiyo ya Trump. Wamesema mabadiiliko hayo ambayo yamewasilishwa baada ya kuuawa kikatili George Floyd hayatakuwa na taathira yoyote katika kuzuia mauaji ya Wamarekani weusi mikononi mwa pilisi.
Seneta Kamala Harris amepinga mabadiliko hayo yaliyotangazwa na Trump kuhusu mabadiliko katika muundo wa Idara ya Polisi Marekani na kusema: "Sisi hatuhitaji ahadi zisizo na chochote, kile ambacho tunahitaji ni mabadiliko ya kimsingi katika mfumo wa polisi Marekani.
Kwa msingi huo mabadiliko ambayo yametangazwa na Trump katu hayataweza kukidhi mataraji ya waliowengi kuhusu kuwazuia maafisa wa polisi Marekani kutumia mabavu dhidi ya raia wa nchi hiyo hasa Wamarekani weusi au wenye asili ya Afrika. Kimsingi amri hiyo ya Trump imetoa mwanya kwa polisi kuendelea kutumia mbinu ya kubinya shingo katika kukabiliana na raia.
Muhimu zaidi ni kuwa, ubaguzi wa rangi umekita mizizi katika muundo wa utawala wa Marekani na moja ya nembo za ubaguzi huo ni ukatili usio na kifani ambao unatumiwa na polisi nchini humo dhidi ya Wamarekani wenye asili ya Afrika.
Kutokana na ubaguzi wa rangi kukita mizizi katika mfumo wa utawala wa Marekani hatuwezi kutarajia hatua za kivitendo zichukuliwe na watawala wa sasa katika kusitisha ukandamizaji na udhalilishaji wa Wamarekani weusi na pia ni wazi kuwa Wamarekani hao wenye asili ya Afrika hawatapewa haki za kijamii ambazo wazungu wanazipata nchini humo.
Kutokana na hali kama hiyo, inatarajiwa kuwa kutaendelea kushuhudiwa hasira na ghadhabu za Wamarekani weusi na Wamarekani wengine wasio wazungu. Hasira hizo zinashuhudiwa sasa katika miji mbali mbali nchini Marekani kupitia maandamano ya wananchi ambao wamepoteza matumaini kuhusu mabadiliko, jambo ambalo wanasiasa wa ngazi za juu nchini Marekani pia wanalikiri. Joe Biden mgombea urais wa chama cha Democrat ambaye atachuana na Trump mwezi Novemba, na ambaye pia alikuwa makamu wa rais wakati wa utawala wa Barack Obama, katika mahojiano na CNN amekiri kuwa kuna ubaguzi wa rangi ulioratibiwa katika jeshi la polisi na mfumo wa utawala wa Marekani. Amesmea: 'Kuna ubaguzi si tu katika muundo wa jeshi la polisi Marekani bali pia katika mfumo wa utawala kunashuhudiwa ubaguzi ulioratibiwa. Kuna ubaguzi kila mahala, katika mfumo wa elimu na katika kazi zote ambazo tunazifanya. Ubaguzi huu ni wa kweli, ni wa kuratibiwa.
Hivi sasa matakwa ya waandamanaji Marekani hayaishii tu katika mabadiliko katika utendaji kazi wa polisi. Kutokana na ukosefu wa usawa na ubaguzi ulio wazi ambao umepelekea kutokuwepo usawa wa fursa baina ya wazungu na weusi, sasa waandamanaji wanataka mabadiliko ya kimsingi katika hali ya kiuchumi na kijamii na kuondolewa ubaguzi na ukosefu wa usawa.