Trump azidi kuandamwa kwa uzembe aliofanya kuhusu COVID-19
Wananchi wa matabaka mbalimbali nchini Marekani wameendelea kumshambulia na kumlaumu vikali rais wa nchi hiyo, Donald Trump kwa uzembe alioufanya wa kushindwa kuchukua tahadhari na hatua zinazotakiwa za kukabiliana na ugonjwa hatari wa corona.
Lawama kali za karibuni kabisa ni zile zilizotolewa na mkuu wa jimbo la Washington ambaye amemlaumu vikali Trump kwa uzembe na uongozi mbovu katika kukabiliana na wimbi la maambukizi ya kirusi cha corona.
Gazeti la Washington Post limemnukuu Jay Inslee akitoa maneno makali dhidi ya Trump ambaye hadi hivi sasa anaendelea kufanya ukaidi wa kutumia barakoa na kung'ang'ania kwake kutetea ubaguzi wa rangi na kulaani wanaovunja masanamu ambayo ni nembo ya utumwa nchini Marekani.
Amemlaumu vikali Trump akisema: Donald Trump hakupaswa kuwataka wafuasi wake wafanye fujo huko Michigan kwani jambo hilo litazidi kuwasha moro wa hitilafu na mapigano zaidi baina ya wafuasi wa Trump na wakuu wa jimbo hilo.
Mwezi uliopita wa Mei 2020, Trump aliwataka wafuasi wake wamiminike mitaani huko Michigan na kukaidi karantini iliyotangazwa na mkuu wa jimbo hilo Gretchen Whitmer ambaye amechukua hatua hiyo kukabiliana na maambukizi makubwa ya corona.
Mkuu wa jimbo la Washington amesisitiza kuwa, hivi sasa Trump anachochea vita na mapigano ya kibaguzi na kikabila katika jamii ya Marekani kwa kuzusha kwake mizozo ya mara kwa mara. Amesema, Trump alipaswa kushughulikia masuala ya kimsingi kama vita dhidi ya ugonjwa wa COVID-19 hasa kwa vile Marekani inaongoza dunia kwa idadi kubwa ya wagonjwa na vifo vya corona lakini badala yake rais huyo anashughulikia masanamu ambayo wapinzani wa ubaguzi wa rangi wanayaangusha chini kulaani kipindi cha utumwa kilichoongozwa na watu waliochongewa masanamu hayo.
Naye Nancy Pelosi, Spika wa Baraza la Congress la Marekani amemlaumu vikali Trump akisema rais huyo ni mfano mbaya sana kwa Marekani.