Mfuko wa Fedha wa Kimataifa wataka jamii ya kimataifa iisaidie Lebanon
(last modified 2020-08-07T08:14:52+00:00 )
Aug 07, 2020 08:14 UTC
  • Mfuko wa Fedha wa Kimataifa wataka jamii ya kimataifa iisaidie Lebanon

Mkurugenzi Mwandamizi wa Mfuko wa Fedha wa Kimataifa IMF jana Alkhamisi alitoa taarifa akiitaka jamii ya kimataifa na nchi rafiki za Lebanon ziisaidie nchi hiyo kupunguza hasara iliyotokana na mlipuko mkubwa uliotokea siku ya Jumanne alasiri katika bandari ya Beirut.

Katika taarifa hiyo Kristalina Georgieva, Mkurugenzi Mwandamizi wa IMF amesema kuwa shirika hilo la kimataifa linatafuta njia zinazowezekana kwa ajili ya kuwasaidia watu wa Lebanon kukabiliana na mkasa huo.

Pamoja na hayo katika hatua ya uingiliaji wa mambo ya ndani ya Lebanon, Georgieva amesema kuwa serikali ya Beirut inapasa kubuni mpango madhubuti wa kutatua mgogoro uliopo wa kiuchumi na kuimarisha misingi ya kuwajibika na kuvutia imani ya wananchi wa nchi hiyo.

Mwezi Mei uliopita pia serikali ya Lebanon ilianzisha mazungumzo na IMF kwa ajili ya kupata mkopo wa kukabiliana na kuenea kwa virusi vya corona na kutatua matatizo ya kiuchumi ya nchi hiyo, jambo ambalo lilishurutishwa kwa serikali ya Beirut kutekeleza marekebisho ya kiuchumi yatakayoziridhisha nchi za Magharibi.

Kristalina Georgieva

Matamshi ya karibuni ya Georgieva yametolewa katika hali ambayo Marwan Aboud, Ganava wa Beirut amekisia hasara iliyosababishwa na mlipuko wa karibuni kuwa kati ya dola bilioni 10 hadi 15.

Jumanne alasiri, mlipuko mkubwa ulitokea katika bandari ya Beirut ambapo kwa mujibu wa takwimu za karibuni, watu zaidi ya 157 wamepoteza maisha na wengine karibu 5000 wamejeruhiwa.

Tags