Marekani yalipigia veto azimio jipya la UN kuhusu magaidi wa kitakfiri
https://parstoday.ir/sw/news/world-i63162-marekani_yalipigia_veto_azimio_jipya_la_un_kuhusu_magaidi_wa_kitakfiri
Marekani imelipigia kura ya veto azimio jipya la Umoja wa Mataifa kuhusu magaidi wa kitakfiri katika kuendelea kushtadi hitilafu kati ya Washington na wanachama wengine wa Baraza la Usalama la umoja huo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Sep 01, 2020 08:20 UTC
  • Marekani yalipigia veto azimio jipya la UN kuhusu magaidi wa kitakfiri

Marekani imelipigia kura ya veto azimio jipya la Umoja wa Mataifa kuhusu magaidi wa kitakfiri katika kuendelea kushtadi hitilafu kati ya Washington na wanachama wengine wa Baraza la Usalama la umoja huo.

Jana Marekani ililipigia kura ya turufu azimio la Umoja wa Mataifa kuhusu mustakbali wa magaidi wa kitakfiri wa nchi ajinabi kwa sababu eti halijalazimisha magaidi hao kurejeshwa katika nchi zao. Azimio hilo liliandaliwa na Indonesa nchi ambayo ni mwanachama asiye wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa. 

Azimio hilo kuhusu magaidi wa kitakfiri lilipigiwa kura 14 za ndio na moja ya hapana. Kelly Craft, Mwakilishi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa ametoa maelezo kuhusu kura ya veto iliyopigwa na nchi yake na kudai kuwa: azimio hilo limefeli kuimarisha mapambano na ndio maana Marekani inakataa kushiriki kwenye kikosi kama hicho kisicho na matumaini. 

Kelly Craft, Mwakilishi wa Marekani UN

Rasimu ya azimio hilo ilikuwa ikielekeza kuwa, magaidi wa kitakifiri wa nchi ajinabi ambao maelfu miongoni mwao wamefungwa jela huko Syria na Iraq wajiunge tena na jamii zao baada ya kukamilisha vifungo vyao hivyo kutoa misaada maalumu kwa  watoto na wake zao.  

Rais Donald Trump wa Marekani huko nyuma pia alitaka kurejeshwa katika nchi zao magaidi wa Daesh raia wa nchi za Ulaya ambao wako jela huko Syria. Ombi hilo la Trump hata hivyo lilipingwa vikali na nchi za Ulaya. 

Hatua ya Marekani ya kupinga azimio hilo jipya la Baraza la Usalama kuhusu magaidi wa kitakfiri inaonyesha kutengwa pakubwa nchi hiyo ndani ya Umoja wa Mataifa. Nchi wanachama wa kudumu na wasio wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa huko nyuma pia zilipinga mipango ya Washington dhidi ya Iran kwa ajili ya kuongeza muda wa vikwazo vya silaha dhidi ya Iran.