Sanders akosoa ubaguzi na dhulma za kiuchumi nchini Marekani
https://parstoday.ir/sw/news/world-i63186-sanders_akosoa_ubaguzi_na_dhulma_za_kiuchumi_nchini_marekani
Seneta wa jimbo la Vermont nchini Marekani amekosoa vikali dhulma na ubaguzi mkubwa wa kiuchumi unaoshuhudiwa nchini humo na kusema kuwa, utajiri wa watu watatu tu wa Marekani unazidi utajiri wa nusu ya jamii ya watu wa nchi hiyo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Sep 02, 2020 23:39 UTC
  • Sanders akosoa ubaguzi na dhulma za kiuchumi nchini Marekani

Seneta wa jimbo la Vermont nchini Marekani amekosoa vikali dhulma na ubaguzi mkubwa wa kiuchumi unaoshuhudiwa nchini humo na kusema kuwa, utajiri wa watu watatu tu wa Marekani unazidi utajiri wa nusu ya jamii ya watu wa nchi hiyo.

Bernie Sanders ameandika katika mtandao wa Twitter kwamba hali mbaya ya kiuchumi nchini Marekani haivumiliki.

Sanders amemkosoa Rais Donald Trump, Kongresi na vyombo vya habari vya Marekani kwa kufumbia macho ubaguzi mkubwa katika masuala ya kiuchumi nchini Marekani. 

Seneta huyo wa jimbo la Vermont amekuwa akikosoa hali mbaya ya Marekani hususan katika kipindi hiki cha maambukizi ya virusi vya corona na kusema: Hali mbaya ya kiuchumi ya Marekani katika utawala wa Trump inaonesha kuwa Wamarekani milioni 29 hawapati chakula cha kutosha na wengine milioni 30 wamepoteza kazi na ajira zao.

Takwimu zinaonesha kuwa uchumi wa Marekani katika kipindi hiki cha maambukizi ya corona umekumbwa na mgogoro mkubwa, na maelfu ya makampuni na viwanda vimefungwa kutokana na athari mbaya za virusi hivyo.

Inakadiriwa kuwa kiwango cha ukosefu wa ajira nchini Marekani kitapanda na kufikia asilimia 16, na kiwango hicho hakijawahi kushuhudiwa nchini humo tangu baada ya mdororo mkubwa wa kiuchumi wa baada ya Vita vya Kwanza vya Dunia.