EU yaiunga mkono Mahakama ya Kimataifa ya Jinai mkabala wa Marekani
https://parstoday.ir/sw/news/world-i63209-eu_yaiunga_mkono_mahakama_ya_kimataifa_ya_jinai_mkabala_wa_marekani
Umoja wa Ulaya umetangaza kuwa unaiunga mkono Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) baada ya serikali ya Marekani kuwawekea vikwazo maafisa wawili wa ngazi za juu wa taasisi hiyo ya kimataifa.
(last modified 2026-02-21T22:51:18+00:00 )
Sep 03, 2020 22:47 UTC
  • Peter Stano
    Peter Stano

Umoja wa Ulaya umetangaza kuwa unaiunga mkono Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) baada ya serikali ya Marekani kuwawekea vikwazo maafisa wawili wa ngazi za juu wa taasisi hiyo ya kimataifa.

Msemaji wa Kamisheni ya Ulaya, Peter Stano amesema kuwa, baada ya hatua ya kushangaza ya Marekani ya kuwawekea vikwazo maafisa wawili wa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai, Umoja wa Ulaya umeieleza Washington upinzani wake dhidi ya hatua hiyo na kusisitiza uungaji mkono wa Brassels kwa taasisi hiyo ya kimataifa. 

Peter Stano amesema kuwa Umoja wa Ulaya unapinga vikali hatua yoyote yenye lengo la kukwamisha mfumo wa haki wa kimataifa na utendaji wa taasisi zake kuu.

Serikali ya Rais Donald Trump wa Marekani Jumatano wiki hii ilitangaza kwamba imewawekea vikwazo vya kiuchumi maafisa wawili wa ngazi za juu wa mahakama hiyo yenye makao yake The Hague nchini Uholanzi.

Donald Trump

Wizara ya Fedha ya Marekani imetangaza kuwa: Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Mahakama ya ICC, Fatou Bensouda na Mkurugenzi wa Mahusiano, Ushirikiano na Mashtaka wa mahakama hiyo, Phakiso Mochochoko wamewekwa katika orodha ya vikwazo ya Marekani. 

Vilevile Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Mike Pompeo amesema kuwa, maafisa wengine wanaoshirikiana na Bensouda watawekewa vikwazo hivyo ikiwa ni pamoja na kunyimwa visa za kuingia Marekani. 

Marekani imechukua hatua hiyo baada ya Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) kuanzisha uchunguzi kuhusu jinai za kivita zilizofanywa na Marekani huko Afghanistan.