Kushadidi migawanyiko ya kisiasa na kijamii Marekani
Kampeni za uchaguzi wa rais wa Marekani zimefika ukingoni. Ikiwa imesalia masaa machache kabla ya uchaguzi mkuu, kumeshuhudiwa majibizano makali baina ya wagombea urais na wafuasi wao na hata katika baadhi ya maeneo kumeripotiwa kuongezeka mapigano ya mitaani baina ya wafuasi wa kambi mbili hasimu za kisiasa.
Wafuasi wa Rais Donald Trump wanaripotiwa kulizingira basi la kampeni la Joe Biden katika jimbo la Texas katika mfano wa hivi karibuni wa makabiliano ya ana kwa ana baina ya wafuasi wa wagombea hao wawili wa uchaguzi mkuu wa Marekani. Trump ameonyesha wazi kufurahishwa na vurugu ambazo ziliibuliwa na wafuasi wake na katika ujumbe wa Twitter amewatetea waibua ghasia hao kwa kusema: "Mimi naipenda Texas."
Hali kadhalika jarida la Axios limefichua kuwa Trump ana mpango wa kujitangaza mshindi katika baadhi ya majimbo muhimu kuanzia Jumanne usiku na iwapo Biden atatangazwa mshindi katika majimbo hayo atawatuhumu Wademocrat kuwa wameiba kura.
Kwa mujibu wa aghalabu ya vyombo vya habari na taasisi zinazohusika na uchaguzi wa Marekani, uhasama wa kisiasa uliopo sasa haujawahi kushuhudiwa katika miongo ya hivi karibuni.
Kundi la Kimataifa la Migogoro limechapisha ripoti kuhusu hatari za mgawanyiko mkubwa Marekani kutokana na uchaguzi na kuandika: "Mapigano ambayo yatapelekea kuvurugika mchakato wa upigaji kura au zoezi la kuhesabu kura yanaweza kushadidi hasa iwapo Trump atadai ushindi na kuwachochea wafuasi wake waandamane kabla ya kukamilika mchakato rasmi wa kuhesabu kura."
Uchochezi huo wa Trump wa kudai kuwepo uwezekano wa wizi wa kura ulianza wiki kadhaa zilizopita. Katika hotuba zake za kampeni, Trump amekuwa akidai mara kwa mara kuwa Biden na wafuasi wake ni Wasosholisti, wanapinga ubepari, wanawapendelea wahamiaji na ni mafisadi na hivyo iwapo watapata ushindi si tu kuwa watahatarisha maslahi ya kitaifa ya Marekani bali pia watapelekea kuangamizwa Ukristo na utambulisho wa kitaifa wa Marekani.
Katika upande wa pili, waungaji mkono wa Biden wanasema Trump na wafuasi wake ni Wafashisti, wabaguzi wa rangi na waibuaji fitina na hivyo iwapo wataendelea kubakia madarakani, Marekani itasambaratika, kutaibuka vita vya wenywe kwa wenywe nchini humo na hivyo kutoa pigo kubwa kwa hadhi ya kimataifa ya nchi hiyo.
Kiwango cha chuki na taasubi baina ya wafuasi wa mirengo yote miwili ni kikubwa kiasi kwamba kuna uwezekano uchaguzi wa mwaka huu wa Marekani utachochea zaidi migawanyiko iliyopo katika jamii ya nchi hiyo.
Migogoro kadhaa imechochea kuzidi kuwa mbaya mgawanyiko wa kisiasa na kijamii huko Marekani. Wamarekani waliowengi, wawe ni Wademocrat, Warepublican au wenye mielekeo huru, wote kwa pamoja hawana imani na mihimili muhimu ya utawala yaani Ofisi ya Rais na Bunge la Kongresi. Usimamizi mbovu na dhaifu katika janga la corona, ukosefu wa ajira na ubaguzi wa rangi ni mambo ambayo yamepelekea kupungua kiwango cha kustahamiliana kisiasa na kijamii Marekani.
Ni kwa msingi huo ndio kinyume na ilivyo ada, katika miaka ya hivi karibuni nchini Marekani kumeshuhudiwa ghasia wakati wa kampeni za uchaguzi, malumbano baina ya wagombea na hata kuwepo jaribio la kumteka gavana wa moja ya majimbo ya nchi hiyo.
Inaelekea kuwa, utendaji mbovu wa viongozi na mihimili ya utawala wa Marekani umepelekea kuwepo mgawanyiko mkubwa wa kisiasa na kijamii na hivyo kuielekeza nchi hiyo katika mgogoro mkubwa na hatari wa kiusalama.