Makumi ya watu watiwa mbaroni katika machafuko ya uchaguzi nchini Marekani
Polisi nchini Marekani wametangaza kuwatia mbaroni makumi ya watu katika jimbo la California katika machafuko ya uchaguzi.
Televisheni ya Russia Today imeripoti habari hiyo na kuongeza kuwa, jimbo la California limetangaza kuwa, watu 40 wametiwa mbaroni katikati ya mji huo baada ya kutanda wasiwasi wa kuzuka fujo na machafuko katika maeneo yote ya Marekani baada ya uchaguzi mkuu wa jana Jumanne.
Televisheni hiyo imeongeza kuwa, mamia ya watu wanaounga mkono kampeni ya "Maisha ya Mtu Mweusi Yana Thamani" wamekusanyika karibu na Ikulu ya Marekani, White House. Watu hao wamepambana na kundi jingine lenye silaha katika eneo hilo.
Wapinzani wa Donald Trump, kuanzia kusini mwa mji wa Washington hadi Seattle, New York na Portland wamefanya maandamano makubwa ya kumlaani rais huyo mchochezi na mbaguzi wa rangi.
Huku hayo yakiripotiwa, timu ya kampeni ya Joe Biden, mgombea wa chama cha Democratic anayechuana na Donald Trump wa chama cha Republican katika uchaguzi huo imemuonya Trump kutokana na vitisho alivyotoa kama atashindwa kwenye uchaguzi huo.
Trump leo amerudia kusema kuwa kama atashindwa hatokubali matokeo na atakwenda mahakamani. Timu ya Kampeni ya Joe Biden imemwambia Trump kwamba timu mbalimbali za wanasheria wa chama cha Democratic ziko tayari kupambana naye iwapo atachukua hatua hiyo.
Hadi wakati tunaandika habari hii, Joe Biden wa chama cha Democratic alikuwa anaongoza kwa kura 238 za Electoral College huku mpinzani wake yaani Donald Trump akiwa amepata kura 213 hadi wakati tunaandika habari hii. Mapema leo Jumatano, Trump amedai kuwa ameshinda uchaguzi huo lakini ameibiwa.