Kujiondoa rasmi Marekani katika Mapatano ya Tabianchi ya Paris
Marekani ambayo imejiondoa katika mikataba kadhaa ya kimataifa wakati wa utawala wa Donald Trump, sasa imejiondoa rasmi katika Makubaliano ya Mabadiliko ya Tabianchi yaliyofikiwa mjini Paris, Ufaransa mwaka 2015. Mapatano hayo ni muhimu katika kulinda mazingira ili kuzuia ongezeko la joto duniani.
Jana Novemba nne Marekani ilitangaza rasmi kujiondoa katika Mapatano ya Kimataifa ya Tabianchi na hivyo kukamilisha mchakato ulioanza mwaka mwaka 2017 wakati Trump alipotangaza nia ya nchi yake ya kujiondoa katika mapatano hayo. Trump alidai kuwa mapatano hayo ya kimataifa ya kulinda mazingira yatasababisha hasara kwa mashirika na walipa kodi wa Marekani. Aidha Trump alisisitiza kuwa, nchi yake iko tayari kurejea katika mapatano hayo iwapo yatabadilishwa kama inavyotaka Marekani. Katika kipindi cha miaka mitatu sasa Trump amekuwa akitumia kila fursa kuyashambulia mapatano hayo.
Mapatano ya Tabianchi ya Paris yalifikiwa katika fremu ya Kongamano la Mfumo wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi (UNFCC) kwa lengo la kupunguza utoaji wa gesi zinachochafua mazingira ambazo aghalabu hutoka katika viwanda. Gesi hizo hupelekea kuwepo mabadiliko katika tabianchi na hasa husababisha ongezeko la joto duniani. Nchi 197 ziliidhinisha mapatano hayo tarehe 12 mwezi Disemba mwaka 2015 mjini Paris.
Marekani ambayo inadai kuwa ni dola kubwa lenye nguvu duniani ni mpinzani mkubwa zaidi wa hatua chanya za kukabiliana na ongezeko la joto duniani. Trump ametangaza bayana kuwa haamini hata kidogo kadhia ya mabadiliko ya tabianchi na ongezeko la joto duniani. Kwa msingi huo, Marekani ambayo yenyewe ni kati ya wachafuzi wakubwa zaidi wa mazingira duniani, imekataa kushiriki katika hatua za kuzuia ongezeko la joto duniani.

Katika miezi ya awali ya urais wake, Trump alitangaza nia ya kujiondoa katika Mapatano ya Tabianchi ya Paris na miaka miwili iliyopita alitia saini amri ya kuondoa nchi yake katika mapatano hayo. Trump alidai kuwa mapatano hayo ya kupunguza joto duniani na kulinda mazingira yatawasababishia hasara wafanyakazi wa viwanda Marekani. Aidha mtawala huyo wa Marekani amesema mapatano hayo ya kulinda mazingira ya dunia yatapelekea hali ya kiuchumi kuwa mbaya zaidi. Ikulu ya White House imedai kuwa Umoja wa Mataifa umefurutu ada katika hatua ambazo uliziwasilisha kukabiliana na uchafuzi wa mazingira. Msimamo huo wa Trump umekosolewa sana ndani na nje ya Marekani.
Abolfazl Zohrevand, mtaalamu wa masuala ya kisiasa anasema, msimamo wa Trump ambao ni msimamo wa mfumo wa kiliberali na kibepari kuhusu Mapatano ya Tabianchi ya Paris, unaonyesha kuwa Marekani ni tishio kwa amani, usalama na mazingira.
Wataalamu wanaonya kuwa, matatizo yanayotokana na ongezeko la joto yanazidi kushadidi kote duniani na hivyo kutishia uhai wa sayari ya dunia. Ongezeko la joto duniani ni chanzo cha kuyeyuka barafu katika ncha ya kaskazini kunakopelekea kuongezeka kiwango cha maji baharini na mafuriko kote duniani na hivyo kuhatarisha maisha ya wengi. Aidha imetabiriwa kuwa, katika maeneo mengi ya nchi, idadi ya vipindi vya joto au mawimbi ya joto yana uwezekano mkubwa wa kupanda na hivyo kusababisha njaa. Kwa msingi huo kuzuia ongezeko la joto duniani ni kati ya maudhui kuu za Umoja wa Mataifa.
Lakini pamoja na hayo,Marekani imekuwa kizingiti kikubwa zaidi katika kukabiliana na uchafuzi wa mazingira ya dunia. Kinyume na anavyodai Trump, Marekani yenyewe pia itakumbwa na madhara ya mabadiliko ya tabianchi na hayo yanashuhudiwa katika joto kali ambalo husababisha misitu kuteketea moto California na majimbo mengine ya magharibi mwa nchi hiyo. Hivyo kujiondoa Marekani katika Mapatano ya Tabia nchi ya Paris ni jambo ambalo litasababisha madhara kwa mazingira kote duniani.