Mpwa wa Trump: Hali Marekani itakuwa hatari sana miezi inayokuja
Mpwa wake rais wa Marekani Donald Trump ametahadharisha kuwa, hali nchini Marekani itakuwa hatari sana katika miezi ijayo kwa sababu Trump hatakubali kushindwa katika uchaguzi.
Katika mahojiano na Televisheni ya MSNBC, Mary Trump amesema mjomba wake hawezi kukubali kushindwa na hivyo miezi inayokuja itakuwa hatari sana. Ametoa wito kwa wakuu wa chama cha Republican wachukue hatua za kumzuia Trump kwani anachochea mapinduzi. Aidha amesema hatua ya Donald Trump kudai kuwa kuna wizi wa kura si sahihi.
Mary Trump ameongeza kuwa, Donald Trump hajawahi kujipata katika hali hii ya kutokuwa na matumani huku akiwa hana uwezo wa kufanya lolote kisheria kuzuia yanayojiri na amebakia mtazamaji tu.
Hivi karibuni Mary Trump alichapisha kitabu kinachofichua ufisaid mkubwa wa Donald Trump.
Hayo yanajiri wakati ambao matokeo ya uchaguzi kutoka majimbo muhimu yenye ushindani yanatarajiwa kutolewa leo, kukiwa na uwezekano wa kubadilisha muelekeo na kusaidia kumpata mshindi wa kinyang'anyiro cha urais kati ya mgombea wa chama tawala cha Republican Rais Donald Trump na mgombea wa chama cha upinzani cha Democratic Joe Biden.
Akizungumza Alhamisi katika Ikulu, Rais Trump aliwashambulia wapinzani wake, akidai wanalenga kufanya udanganyifu dhidi yake. Kwa upande wake, Biden amedokeza kuwa kura hizo zinahitaji muda wa kujumlishwa huku akisema ana uhakika kuwa ataibuka mshindi.