Wademocrati waanza kusherehekea ushindi, Biden akaribia zaidi White House
Mgombea urais wa Marekani kwa tiketi ya chama cha Democratic, Joe Biden anaendelea kumtimulia kivumbi mpinzani wake wa chama cha Republican, Donald Trump katika matokeo ya uchaguzi wa rais wa Marekani kwenye majimbo mawili muhimu ya Pennsylvania na Georgia ambayo huenda yakamkabidhi rasmi Biden ufunguo wa kuingia Ikulu ya White House.
Baada ya kuhesabiwa asilimia 96 ya kura zote zilizopigwa, ngombea wa chama cha Democratic, Joe Biden alikuwa akiongoza kwa kura nyingi na kumuacha nyuma Donald Trump. Televisheni ya CNN ya Marekani imeripoti kuwa Biden amemuacha nyuma Trump kwa zaidi ya kura elfu 14 na 500 katika jimbo la Pennsylvania peke yake.
Ushindi wa Biden katika jimbo hilo lenye kura 20 za wajumbe wa Electoral College utatosha kumtangaza rasmi kuwa rais mpya wa Marekani.
Huko Philadelphia wafuasi wa chama cha Democratic wameanza kusherehekea ushindi wa mgombea wa chama hicho, Joe Biden kwa nderemo na vifijo. Biden anatarajia kuhutubia Wamarekani muda wowote, na inatazamiwa kuwa itakuwa hotuba ya ushindi.
Katika jimbo la Georgia, Kituo cha Utafiti cha Edison kimetangaza kuwa Joe Biden amezidi kumtimulia kivumbi Trump kwa kura 4,263. Wakati huo huo Spika wa Kongresi ya Marekani, Nancy Pelosi amesema kuwa, Joe Biden anaelekea kushinda uchaguzi wa rais.
Pelosi ametumia neno "rais mteule Joe Biden" akimaanisha kuwa mgombea huyo wa chama cha Democratic ameshinda kinyang'anyro hicho.
Sambamba na hayo yote, vyombo vya habari vya Marekani vinaeleza kuwa taasisi za usalama na upelelezi za nchi hiyo zimezidisha ulinzi wa Biden kadiri anavyokaribia zaidi mlango wa White House.
CNN pia imetangaza kuwa Mamlaka ya Usafiri wa Anga ya Marekani imezuia ndege kuruka katika anga ya juu ya nyumba Joe Biden na kituo cha timu yake ya kampeni za uchaguzi katika jimbo la Delaware.
Katika upande mwingine Donald Trump ameendelea kudai kuwa zoezi la kuhesabu kura za uchaguzi wa rais wa Marekani limegubikwa na udanganyifu mkubwa na kwamba amewasilisha mashtaka katika Mahakama Kuu ya Federali. Trump pia amemtahadharisha mpinzani wake, Joe Biden asijitangazie ushindi na kutishia kuwa iwapo atafanya hivyo yeye pia atajitangaza mshindi katika uchaguzi wa rais wa Marekani.