Uwezekano wa Biden kuendeleza sera za kivita za Marekani
Afisa wa zamani wa Shirika la Usalama na Ushirikiano la Ulaya (OSCE) ametahadharisha kuwa, kwa kuzingatia historia ya chama cha Democrat, kuna uwezekano mkubwa kuwa sera za kivita za Marekani zitaendelea wakati wa urais wa Joe Biden.
Willy Wimmber, naibu mkuu wa zamani wa Shirika la Usalama na Ushirikiano la Ulaya amesema kuna uwezekano mkubwa kuwa, chini ya uongozi wa Biden, Marekani itaanza vita katika nchi za kigeni.
Afisa huyo wa zamani wa OSCE ameongeza kuwa, Biden hataingia peke yake katika Ikulu ya White House bali ataandamana na wanasiasa wa chama chake cha Democrat ambacho katika muongo wa 1990 kiliangamiza hati ya Umoja wa Mataifa.
Mwanasiasai huyo mkongwe wa Ujerumani ameashiria kitendo cha muungano wa kijeshi wa NATO, chini ya uongozi wa Marekani, cha kudondosha mabaomu Yugoslavia ya zamani wakati utawala wa Bill Clinton mwaka 1999. Aidha amesema katika zama za urais wa Barack Obama, Biden alikuwa makamu wa rais na aliafiki kitendo cha Obama cha kuendesha vita Asia Magharibi kwa kutumia ndege zisizo na robani. Kwa msingi huo kuna uwezekano mkubwa kuwa Biden atatumia mbinu za Wademocrat za muongo wa 1990 na pia sera ambazo Obama alitumia wakati wa urais wake.
Hayo yanajiri wakati ambao bado mgogoro unaendelea kutotoka nchini Marekani baada ya Joe Biden kutangazwa mshindi wa uchaguzi wa rais huku Rais Donald Trump akipinga matokeo hayo kwa madai kuwa uchaguzi uligubikwa na wizi wa kura.