Mapigano baina ya wapinzani na waungaji mkono wa Trump mjini Washington
Maandamano ya wafuasi na waungaji mkono wa Rais Donald Trump wa Marekani wanaopinga matokeo ya uchaguzi wa rais uliofanyika tarehe 3 mwezi huu wa Novemba yameufanya mji wa Washington kuwa uwanja wa mapaigano baina ya wafuasi na wapinzani wa kiongozi huyo.
Katika mandamano hayo ya maelfu kadhaa ya wafuasi wa Trump kulitokea mapigano makali baina yao na wapinzani wa kiongozi huyo. Waungaji mkono wa Trump katika maandamano ya jana mjini Washington waliongozwa na baadhi ya makundi yenye misimamo mikali ya mrengo wa kulia kama lile linalojiita Proud Boys. Inasemekana kuwa upande wa upinzani uliongozwa na kundi la ANTIFA (Anti-fascism).
Donald Trump alikuwa amewataka waungaji mkono wake wafanye maandamano katika miji mbalimbali ya Marekani ukiwemo Washington kupinga matokeo ya uchaguzi wa rais ambao anadai umegubikwa na udanganyifu. Trump aliyeshindwa katika kura za wananchi na vilevile katika kura za wajumbe wa Electoral College, ameandika kwenye ukurasa wa Twitter kwamba: Mamia ya maelfu ya Wamarekani wameandamana Washington DC na kuonyesha kwamba, hawawezi kustahamili uchaguzi mbovu na uliogubikwa na udanganyifu."
Hii ni licha ya kwamba, vyombo vya juu kabisa vya usimamizi wa uchaguzi wa rais nchini Marekani vimetangaza kuwa, uchaguzi wa mwaka huu ndio uliokuwa salama zaidi na haukuwa na udanganyifu wala uchakachuaji wa kura. Taarifa za mara kwa mara za wasimamizi wa uchaguzi wa rais na maafisa mbalimbali wa majimbo ya Marekani wakisisitiza kuwa zoezi hilo limefanyika vizuri na bila ya udanganyifu, hazikuweza kumzuia Trump na waungaji mkono wake kutoa madai ya kufanyika udanganyifu katika uchaguzi wa rais. Trump angali anasisitiza kuwa, anamini ataibuka mshindi katika kinyang'anyiro hicho licha ya taarifa za awali kuonesha kuwa, mpinzani wake wa chama cha Democratic, Joe Biden ameshinda kwa kupata kura nyingi za wananchi na za wajumbe wa Electoral College.
Inaonekana kuwa Donald Trump anategemea sana maamuzi ya mahakama, wajumbe wa Electoral College, na zaidi yote, anategeme machafuko ya wafuasi wake katika mitaa na barabara za miji ya Marekani ambao aghlabu yao wana misimamo mikali na wamejizatiti kwa silaha moto. Suala hilo limemfanya mshauri wa zamani wa usalama wa taifa wa Trump, John Bolton awatahadharishe maafisa wa chama cha Republican na kusisitiza kuwa: "Iwapo chama cha Republican kitakataa kumuweka kando Trump na kumkubali Joe Biden kama rais mteule, basi chama hicho kitalipa gharama kubwa za kisiasa."
Seneta wa kujitegemea wa Marekani, Bernie Sanders pia ametahadharisha kuhusu msimamo wa sasa wa Trump na baadhi ya viongozi wakuu wa chama cha Republican kuhusu suala la kutokubali matokeo ya uchaguzi wa rais na kusema: "Hatua ya viongozi wa Republican ya kukataa matokeo ya uchaguzi wa rais si shambulio dhidi ya Biden peke yake, la hasha, bali ni shambulizi dhidi ya demokrasia ya Marekani na kielelezo cha azma ya chama cha Republican ya kutaka kutwaa madaraka."
Katika siku za hivi karibuni baadhi ya wapinzani wa Donald Trump wameenda mbali zaidi na kumfananisha kiongozi huyo wa Marekani na dikteta wa zamani wa Ujerumani, Adolf Hitler, na kwamba wafuasi wake mafashisti.
Tukiachilia mbali bwabwaja za Trump na wafuasi wake, kwa saa Marekani imetumbukia katika hali ya machafuko na ukosefu wa utulivu kutokana na migogoro mingi ya kisiasa, kiuchumi na kijamii inayoizonga nchi hiyo. Haya yote yanaambatana na kasi kubwa ya maambukuzi ya virusi vya corona ambavyo hadi sasa vimeua malaki ya Wamarekani na kusababisha matatizo mengi ya kiuchumi na ukosefu wa ajira kwa mamilioni ya raia wa nchi hiyo.