Polisi ya Ufaransa yatumia mkono wa chuma kukandamiza maandamano ya wananchi
Maelfu ya waandamanaji nchini Ufaransa wamekabiliana na polisi kwenye mji mkuu wa nchi hiyo Paris, haya yakiwa ni maandamano mapya kupinga muswada wa sheria tata kuhusu usalama.
Polisi walilazimika kutumia mabomu ya kutoa machozi baada ya waandamanaji waliofunika nyuso zao kuanza kuvunja maduka na kuchoma moto magari kadhaa.
Mbali na mji mkuu Paris, maandamano kama hayo yalishuhudiwa pia katika zaidi ya miji 90 ambao raia walijitokeza kupinga muswada wa sheria tata ambao utakataza watu kuwarekodi picha za video polisi wakati wakikabiliana na waandamanaji.
Wapinzani wa muswada huo wanasema utaminya uhuru wa vyombo vya habari na kuruhusu unyanyasaji wa polisi dhidi ya raia.
Ufaransa imekuwa ikishuhudia maandamano ya kila wiki kupinga muswada huo, ambapo maandamano hayo yalishadidi zaidi baada ya kuonekana kwa picha za video zikiwaonesha polisi wakimpiga vibaya kijana mmoja mwenye asili ya Kiafrika.
Licha ya serikali ya Ufaransa kutangaza kuwa, imefutilia mbali muswada huo iliokuwa imeuwasilisha bungeni kwa ajili ya kupiga marufuku upigwaji picha maafisa wa polisi wanapokuwa wanatekeleza majukumu yao,lakini waandamanaji wameendelea kuandamana.
Maelfu ya waandamanaji wakiwemo wale wa vizibao vya njano waliokuwa wanaipinga Serikali wameshiriki maandamano ya mwishoni mwa juma hili, ambapo baada ya kutokea kundi la waandamanaji waliofunika nyuso zao na kuanza kuharibu mali, ndipo polisi walilazimika kutumia nguvu kuwakabili waandamanaji.