France 24 yakosoa undumakuwili wa Macron kuhusu haki za binadamu
https://parstoday.ir/sw/news/world-i65158-france_24_yakosoa_undumakuwili_wa_macron_kuhusu_haki_za_binadamu
Serikali ya Ufaransa inaendelea kukosolewa kwa kuchukua misimamo inayokinzana na madai yake ya kutetea haki za binadamu kutokana na kuonyesha undumakuwili juu ya suala hilo kwa kuendelea kuziuzia silaha tawala kandamizi.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Dec 12, 2020 22:16 UTC
  • France 24 yakosoa undumakuwili wa Macron kuhusu haki za binadamu

Serikali ya Ufaransa inaendelea kukosolewa kwa kuchukua misimamo inayokinzana na madai yake ya kutetea haki za binadamu kutokana na kuonyesha undumakuwili juu ya suala hilo kwa kuendelea kuziuzia silaha tawala kandamizi.

Katika ripoti inayotoa changamoto kwa msimamo wa kiundumakuwili wa serikali ya Paris wa kuziuzia silaha tawala kandamizi na za kidikteta, tovuti ya kanali ya televisheni ya France 24 imeandika kuwa, safari ya karibuni ya Rais Abdel Fattah el Sisi wa Misri mjini Paris na mapokezi mazuri aliyopewa na Rais Emmanuel Macron ni ithbati kwamba Ufaransa haishughulishwi hata kidogo na lawama za fikra za waliowengi wala ukosoaji na malalamiko dhidi ya ukiukaji wa haki za binadamu unaoendelea kufanywa na serikali ya Misri; na kwa hivyo inaendelea kama kawaida kuuuzia silaha utawala wa Cairo na tawala kandamizi nyinginezo.

Hayo yanafanyika wakati faili la haki za binadamu la utawala wa rais Abdel Fattah el Sisi wa Misri linaendelea kuwa chafu zaidi siku baada ya siku.

Rais Abdel Fattah el Sisi wa Misri

Kwa mujibu wa ripoti hiyo ya France 24, wakati Macron anakabiliwa na tuhuma za kuminya haki za kiraia za Wafaransa na kupungua uwazi katika utendaji wake, safari ya karibuni ya el Sisi nchini humo imethibitisha kuwa Ufaransa imeamua kurejea kwenye mwenendo wake wa zamani wa kufumbia macho dhulma zinazofanywa na nchi inazofanya nazo biashara ya kuziuzia silaha.

Vipimo vinavyogongana na vya undumakuwili vinavyotumiwa na madola ya Magharibi kuhusiana na masuala ya haki za binadamu vimekuwa vikiibua mijadala kila mara katika duru za wakosoaji wa kisiasa.../