Trump atafakari kutumia jeshi kubatilisha matokeo ya uchaguzi
https://parstoday.ir/sw/news/world-i65296-trump_atafakari_kutumia_jeshi_kubatilisha_matokeo_ya_uchaguzi
Rais Donald Trump wa Marekani amefanya mashauriano na wapambe wake kuhusu uwezekano wa kutumia jeshi kubatilisha matokeo ya uchaguzi.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Dec 20, 2020 03:36 UTC
  • Trump atafakari kutumia jeshi kubatilisha matokeo ya uchaguzi

Rais Donald Trump wa Marekani amefanya mashauriano na wapambe wake kuhusu uwezekano wa kutumia jeshi kubatilisha matokeo ya uchaguzi.

Kufuatia mapendekezo la baadhi ya mafisa wa Marekani kwa Donald Trump kuwa anaweza kutangaza utawala wa kijeshi ili abatilishe matokeo ya uchaguzi, sasa rais huyo ambaye amekataa kushindiwa amefanya mashauriano na watu kadhaa kuhusu utekelezwaji wa mpango huo.

Imedokezwa kuwa Trump amefanya mazungumzo na baadhi ya washauri na waitifaki wake, ambapo suala hilo la kuanzisha utawala wa kijeshi limejadiliwa kwa kina. 

Hiyo juzi mshauri wa zamani wa usalama wa taifa wa Marekani, amemshauri rais wa nchi hiyo, Donald Trump atangaze serikali ya kijeshi ili aweze kulazimisha kurejewa uchaguzi wa rais nchini humo.

Joe Biden

Michael Flynn amesema hayo katika mahojiano aliyofanyiwa na Newsmax Media na kuongeza kuwa, kama Trump atataka, anaweza kutuma vikosi vya kijeshi katika majimbo tofauti ya Marekani na kulazimisha kurudiwa uchaguzi wa rais katika maeneo ambayo anahisi ameibiwa kura.

Viongozi wa ngazi za juu Marekani wana wasiwasi kuwa, Trump sasa anatumia vibaya mamlaka yake ili abadilishe matokeo ya uchaguzi. 

Hayo yanajiri katika hali ambayo, matokeo ya uchaguzi wa rais wa Marekani ya Novemba 3, 2020 yalipasishwa na  Wajumbe wa Uchaguzi wanaojulikana kama Electoral College siku ya Jumatatu ya tarehe 14 Disemba na kumtangaza rasmi Joe Biden kuwa rais mpya wa Marekani.

Trump anadai kumetokea wizi mkubwa wa kura katika uchaguzi wa rais na amewasilisha malalamiko mahakamani lakini malalmiko yake yote yametupiliwa mbali.