Trump: White House na Seneti hazitaingia kwenye mikono ya Wademocrat
https://parstoday.ir/sw/news/world-i65593-trump_white_house_na_seneti_hazitaingia_kwenye_mikono_ya_wademocrat
Kwa mara nyingine tena Rais Donald Trump wa Marekani amekataa kuyakubali matokeo ya uchaguzi wa rais wa nchi hiyo uliofanyika Novemba 3 mwaka uliopita, ambayo yanaonyesha kuwa ameshindwa.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jan 05, 2021 03:42 UTC
  • Trump: White House na Seneti hazitaingia kwenye mikono ya Wademocrat

Kwa mara nyingine tena Rais Donald Trump wa Marekani amekataa kuyakubali matokeo ya uchaguzi wa rais wa nchi hiyo uliofanyika Novemba 3 mwaka uliopita, ambayo yanaonyesha kuwa ameshindwa.

Akihutubia wafuasi wake katika jimbo la Georgia, Trump amedai kuwa Ikulu ya White House na Baraza la Seneti hazitaingia kwenye mikono wa Wademocrat.

Aidha amekariri madai yake ya kufanyika udanganyifu mkubwa katika uchaguzi wa rais wa Marekani na akasisitiza kwamba "Wademokrati wa Kiliberali" hawataihodhi Ikulu ya White House.

Katika hotuba yake hiyo, rais huyo wa Marekani vilevile amesema, ana matumaini makamu wake Mike Pence ataitumia nafasi yake akiwa mwenyekiti wa Baraza la Seneti kumsaidia yeye kwa ajili ya kubadilisha matokeo ya uchaguzi.

Trump (kushoto) na makamu wake Mike Pence

Hadi sasa Maseneta 11 wa chama cha Republican wametangaza kuwa hawana nia ya kupinga ushindi wa mgombea urais kwa tiketi ya chama cha Democratic Joe Biden katika kikao cha kumuidhinisha rais huyo mteule.

Baraza la Seneti la Marekani litafanya kikao kesho Jumatano, Januari 6 kwa uenyekiti wa Makamu wa Rais Mike Pence ili kutangaza matokeo ya kura za Jopo la Wawakilishi Wateule wa Majimbo, linalojulikana kama Electoral College.../