Trump adai kuchakachuliwa kura katika uchaguzi mdogo wa Georgia
Rais wa Marekani amekituhumu chama cha Democratic kuwa kimefanya udanganyifu katika uchaguzi mdogo wa Baraza la Sanate la nchi hiyo.
Donald Trump leo Jumatano ameandika katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Twitter kwamba Wademocrat wameandaa idadi kubwa ya wapiga kura hewa ili waweze kuwashinda wagombea wa chama cha Republican. Je, wanadhani wanaweza kupata kura za kukishinda chama cha Republican?
Chini ya masaa mawili baadaye Trump ameandika tena kwamba: "Tazama! Sasa hivi kura 4000 zilizotumwa kwa njia ya posta zimepatikana katika Kaunti ya Fulton!"
Matokeo ya awali na yasiyo rasmi ya uchaguzi mdogo wa Baraza la Sanate katika jimbo la Georgia yanaonesha kuwa, mgombea wa chama cha Democratic, Raphael Warnock, amempiku mgombea wa chama cha Trump cha Republican kwa kupata kura 35,000 zaidi na hivyo ameshinda kiti hicho.
Mgombea mwengine wa chama cha Democratic anayeitwa Joh Ossof naye amempiku kwa kura mgombea wa Baraza la Sanate wa chama cha Trump cha Repblican, David Perdue, katika uchaguzi huo mdogo.
Hatima ya chama chenye viti vingi katika Baraza la Sanate wakati wa Rais Joe Biden huko Marekani inategemea uchaguzi huo mdogo wa Georgia.
Hadi hivi sasa pia Donald Trump analalamikia uchakachuaji mkubwa wa kura katika uchaguzi wa rais wa Novemba 3, 2020, uliompa ushindi Joe Biden. Mahakama za Marekani, kubwa na ndogo zote zimekataa madai ya Trump kutokana na kukosekana ushahidi wa kuthibitisha madai yake hayo.