Marekani katika lindi la machafuko ya kisiasa
Machafuko, fujo, vurugu, uporaji, ufyatuaji risasi, mauaji, ugaidi, mapinduzi, kukabiliana na mapinduzi; bali kwa kifupi; kashfa ya taifa, ndiyo maneno ambayo kila moja linafasiri matukio ya aibu yaliyotokea jana Jumatano, Januari 6, 2021 nchini Marekani ndani jengo la Congress
Matukio yote hayo yalitarajiwa kwani mambo yaliyojiri hivi karibuni ya kisiasa nchini Marekani, kuanzia uchaguzi mdogo wa maseneta wawili wa Georgia hadi kikao cha Congress cha jana Jumatano tarehe 6 Januari 2021 cha kupasisha ushindi wa Joe Biden katika uchaguzi wa rais wa Novemba 3, 2020 yamezidi kuonesha mvurugano uliopo baina ya wanachama wa vyama viliwi vikuu vya Marekani vya Democratic na Republican.
Uchaguzi mdogo wa maseneta wa jimbo la Georgia uliofanyika tarehe 5 mwezi huu wa Januari 2021, umekipa ushindi chama cha rais mteule Joe Biden cha Democratic, baada ya wagombea wote wawili wa chama hicho kuwapiga na chini wagombea wa chama cha Republican cha rais aliyebwagwa, Donald Trump.Kabla ya uchaguzi huo, Warepublican walikuwa na viti 50 katika Baraza la Sanate. Lakini baada ya Wademocrat kushinda viti viwili vya Georgia, Warepublican hawana tena wingi wa viti katika baraza hilo. Idadi ya maseneta imekuwa sawa baina ya vyama hivyo viwili na sasa kura za Kamala Harris, Makamu wa Rais wa baadaye wa Marekani na Spika wa Baraza la Sanate la nchi hiyo zitakuwa muhimu mno katika maamuzi wa Baraza la Sanate.

Amma tukija katika upande mwingine tutaona pia kwamba vurugu, machafuko, mauaji na uvamizi ulioambatana na kikao cha jana Jumatano cha Baraza la Congress cha kupasisha ushindi wa Biden katika ucahguzi wa rais kilidhihirisha mzozo na mvurugano mkubwa baina ya Warepublican na Wademocrat na katika jamii nzima ya Marekani. Rais wa hivi sasa wa Marekani, Donald Trump mwenye vituko na kelele nyingi, amepigwa mweleka na Joe Biden, lakini hadi hivi sasa amekataa kushindwa, bado ana tamaa ya kubadilisha matokeo ya uchaguzi na amewachochea wafuasi wake wafanye maandamano na fujo katika mji mkuu Washington DC kupinga matokeo ya uchaguzi wa rais na matokeo yake ni vitendo vya aibu na kashfa ya taifa ima la Marekani vya jana Jumatano. Siku chache zilizopita pia kulifichuliwa mazungumzo ya simu kati ya Trump na afisa mmoja wa jimbo la Georgia akimshinikiza abadilishe matokeo ya kura za jimbo hilo, na hiyo imekuwa ni fedheha na kashfa kubwa kwa Trump.
Alexandria Ocasio-Cortez, mbunge wa chama cha Democratic huko Marekani anasema: Simu hiyo ya Trump na hatua yake ya kumshinikiza waziri wa jimbo la Georgia abadilishe kura kwa manufaa yake Trump, ni uhalifu ambao unastahiki rais huyo wa Marekani aitwe bungeni kujieleza.

Hatua ya Trump ya kuwachochea wafuasi wake wapenda fujo, wakiwemo wa genge la kikatili la mrengo wa kulia linalojiita "Vijana Maghururi" ili wakusanyike na kufanya fujo mjini Washington na hatimaye kuukumbi wa Congress na kufikia hata kufanya mauaji, kumezidi kuchochea machafuko katika mji mkuu huo wa Marekani. Zaidi ya hayo, Trump amezidisha mno kampeni zake nalicha ya kupigwa na chini mtawalia katika kesi zake mahakamani lakini bado anapiga ngoma ya kuweko udanganyifu mkubwa katika uchaguzi wa Marekani. Hata hivyo nukta muhimu zaidi ni kwamba, karibu maseneta 11 na wabunge 140 wa chama cha Republican wametangaza kuunga mkono madai ya Trump na jambo hilo limezidi kukitia kwenye mizozo kikao cha Baraza la Congress cha kupasisha ushindi wa Joe Biden.
Ilijulikana tangu zamani kwamba Warepublican hawana uwezo wa kubadilisha ushindi wa Joe Biden hasa baada ya Electoral Colledge kuupasisha uchaguzi wa Novemba 3, 2020. Pamoja na hayo baadhi ya Warepubalican wanavichukulia vita vyao na Wademocrat kuwa vitawafaa kisiasa, vitawapa umaarufu na vitaonesha bado wana nguvu.

Ni jambo lililo wazi kwamba, ushindi wa chama cha Democratic katika uchaguzi mdogo wa Georgia pamoja na katika kupasishwa urais wa Joe Biden katika baraza la Congress hauna maana kabisa ya kumalizika mizozo na mivurugano ya kisiasa nakiuchaguzi baina ya Wademocrat na Warepublican huko Marekani. Bado chama cha Republican kina viti vya kutosha ndani ya Baraza la Sanate vya kuweza kukwamisha maamui ya Wademocrat hasa kwa kuzingatia kuwa kiwango cha chini kabisa cha kupasishwa miswada katika baraza hilo, ni kuta 60 za ndio za wajumbe wa baraza hilo. Tab'an mivutano baina ya vyama hivyo viwili vya Marekani imekuwepo muda wote na ni rahisi kutabidi kwamba mizozo itaendelea pia wakati wa urais wa Joe Biden huko Marekani.