Mgogoro wa usalama nchini Marekani
https://parstoday.ir/sw/news/world-i65727-mgogoro_wa_usalama_nchini_marekani
Uvamizi uliofanywa na wafuasi wa Donald Trump dhidi ya jingo la Kongresi ya Marekani Januari sita mwezi huu na tishio la kuendelea vitendo kama hivi vya utumiaji mabavu sambamba na kujiuzulu maafisa wa usalama wa nchi hiyo, ni mambo ambayo yameifanya Marekani ikabiliwe na mgogoro wa usalama wakati huu wa kukaribia hafla ya kuapishwa rais mteule wa nchi hiyo Joe Biden.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Jan 12, 2021 12:30 UTC
  • Mgogoro wa usalama nchini Marekani

Uvamizi uliofanywa na wafuasi wa Donald Trump dhidi ya jingo la Kongresi ya Marekani Januari sita mwezi huu na tishio la kuendelea vitendo kama hivi vya utumiaji mabavu sambamba na kujiuzulu maafisa wa usalama wa nchi hiyo, ni mambo ambayo yameifanya Marekani ikabiliwe na mgogoro wa usalama wakati huu wa kukaribia hafla ya kuapishwa rais mteule wa nchi hiyo Joe Biden.

Katika tukio la hivi karibuni kabisa, ni kujiuzulu Chad Wolf, Kaimu Waziri wa  Wizara ya Usalama wa Ndani ya Marekani zikiwa zimebakia siku nane tu kabla ya kufanyika hafla ya kumuapisha Rais mpya. Chad Wolf amesema kuwa, matukio ya hivi karibuni nchini Marekani likiwemo tukio la wafuasi wa Trump kuvamia Kongresi ya nchi hhiyo ndio sababu iliyomfanya ajiuzulu wadhifa wake huo.

Kabla ya hapo Wolf alikuwa amemtaka Trump alaani utumiaji mabavu uliofanywa wakati wa kuvamia jengo la Kongresi kama sharti la kubakia katika nafasi yake. Kujiuzulu Chad Wolf sambamba na mlolongo wa kujiuzulu maafisa wengine wa ngazi za juu nchini humo, kunahesabiwa kuwa pigo kubwa kwa itibari ya Trump katika siku hizi za mwisho za kuweko kwake katika Ikulu ya White House.

Wakati huo huo, kujiuzulu Chad Wolf, Kaimu wa Wizara ya Usalama wa Ndani ni ishara ya wazi ya kuweko ombwe la wazi katika uga wa kulinda usalama hasa katika kipindi cha siku hizi nyeti na zenye mgogogo. Hasa kwa kutilia maanani kwamba, matukio ya sasa ya nchi hiyo yanaashiria kutokea tufani kubwa katika siku za zijazo. Kanali ya Televisheni ya Fox News inaripoti kuwa, Wizara ya Usalama wa Ndani, ndio asasi kuu yenye jukumu la kudhamini usalama katika hafla ya kuapishwa Joe Biden. Hivyo kujiuzulu kwa Chad Wolf kunaweza kuwa na taathira hasi kwa mipango ya kiusalama tarehe 20 mwezi huu siku ambayo Biden ataapishwa na kuchukua rasmi hatamu za uongozi wa nchi hiyo.

Donald Trump

 

Mustakabali wa hali ya usalama nchini Marekani unakabiliwa na giza hasa kwa kuzingatia vitisho vya mara kwa mara vya makundi ya wanamgambo wenye silaha wanaomuunga mkono Trump vya kuanzisha machafuko na vurugu za barabarani. Polisi ya Federali (FBI) imesema kuwa, imepokea taarifa za kipelelezi kuhusiana na kundi la wabeba silaha ambalo limepanga kufanya safari tarehe 16 mwezi huu kuelekea Washington. Kundi hilo limetoa onyo kwamba, endapo Kongresi ya nchi hiyo itafanya juhudi za kumuondoa madarakani kwa kutumia kipengee kamilishi nambari 25 cha katiba ya nchi, basi ardhi ya nchi hiyo itashuhudia vurugu na machafuko makubwa. Imekuja katika ripoti ya FBI kwamba: Kumeandaliwa mipango ya kufanyika maandamo ya silaha mbele ya majengo ya Mabunge yote ya majimbo 50 ya Marekani kuanzia tarehe 16 hadi 20 mwezi huu na katika mji mkuu wa nchi hiyo kuanzia tarehe 17 hadi 20 ya mwezi huu wa Januari.

Katika kipindi cha sasa si tu kwamba, Marekani inakabiliwa na mgogoro wa kisiasa ambao haujawahi kushuhudiwa, bali mgogoro wa usalama nao umeigubika nchi hiyo. Ukweli wa mambo ni kuwa, mgogoro wa sasa wa Marekani umekuwa ukichukua mkondo mpana zaidi siku baada ya siku katika uga wa ndani na kimataifa pia.

Donald Trump ameendelea kung'ang'ania msimamo wake kwamba, uchaguzi uliopita ulitawaliwa na wizi na udanganyifu, licha ya kuonekana kulegeza kamba msimamo wake huo kiujanja baada ya tukio la uvamizi wa wafuasi wake dhidi ya jengo la Kongresi, ambapo amesema yuko tayari kukabidhi madarakani kwa Joe Biden na hatajiuzulu mpaka akamilishe muda wake wa uongozi. Hii ni katika hali ambayo, matakwa na mashinikizo ya kujiuzulu Trump yameshadidi mno.

Joe Biden, Rais mteule wa Marekani

 

Wakati huo huo, wafuasi wa Trump wenye kupenda kufanya machafuko na fujo katika jamii ya Marekani ambayo imegawanyika katika kambi mbili, wangali wanasisitiza kuendelea kumuunga mkono kiongozi huyo hata kwa gharama ya kuibuka machafuko ya utumiaji silaha katika majimbo yote 50 ya nchi hiyo. Tajiriba ya tukio la kuvamiwa Kongresi hivi karibuni imeonyesha kuwa, vikosi vya polisi havina uwezo wa kukabiliana na watu hao na makundi ya wanamgambo wabeba silaha. Ni kutokana na ukweli huo, ndio maana serikali ya kifederali haina budi isipokuwa kuwatumia askari wa Gadi ya Taifa. Kama ambavyo Gadi ya Taifa ya Marekani imetangaza kuwa, askari 15,000 wanatarajiwa kusimamia amani katika hafla ya kuapishwa Joe Biden.

 Pamoja na hayo, inawezekana kutabiri kwamba, shughuli hiyo huenda ikakumbwa na vurugu na machafuko kutokana na kuweko maelfu ya wafuasi wa Trump katika mji wa Washington DC. Katika mazingira kama hayo, demokrasia ya Marekani itakuwa imekumbwa na fedheha mpya. Kwa maneno mengine ni kuwa, Trump na mamilioni ya wafuasi wake hawako tayari kukubaliana na chaguo la wengi la wananchi wa nchi hiyo ambao wamemchagua Biden kwa kura milioni 85. Na wakiwa na nia ya kufikia lengo lao wako tayari hata kuitumbukiza jamii ya nchi hiyo katika vurugu na machafuko.

Steve Schmidt, mwanastratejia wa zamani wa Warepulican anasema kuwa, watu wenye fikra za Ki-trump na kijumla fikra ya U-trump ni harakati ya kiudikteta ambayo ina ishara za ufashisti. Bila shaka itakuwa ni aibu na udhalili mkubwa kwa Marekani kama itashindwa kudhibiti hali ya usalama wake wa ndani, katika hali ambayo, ndio nchi pekee duniani yenye kutumia gharama kubwa katika masuala ya kijeshi.