Jan 17, 2021 02:21 UTC
  • Pelosi: Wote waliochochea na kuongoza kuvamiwa Congress ya Marekani watafuatiliwa kisheria

Spika wa Baraza la Wawakilishi la Marekani amesema kuwa, yeyote aliyehusika na kuvamiwa jengo la Congress la nchi hiyo hata kama ni mbunge atafuatiliwa kisheria.

Nancy Pelosi amesema hayo mbele ya waandishi wa habari na kujibu swali lililosema, je, kama kuna wabunge wa Marekani wamechochea kuvamiwa jengo la Congress hapo tarehe 6 Januari 2021, nao watachukuliwa hatua, akisema, kama itathibitika wabunge wamehusika katika fitna na uvamizi huo, basi hatua kali zitachukuliwa dhidi yao.

Matamshi hayo ya spika wa bunge la Marekani yametolewa huku kukiwa na habari kwamba mbunge wa chama cha Democratic, Mikie Sherrill amewatuhumu baadhi ya wabunge wa chama cha Republican kuwa waliwachochea wafuasi wa Trump kuvamia jengo la Congress bali baadhi ya wabunge hao waliongoza makundi ya wavamizi siku moja kabla ya kuvamiwa jengo la Congress tarehe 6 Januari 2021 mjini Washington DC.

Magenge ya Donald Trump yalipovamia jengo la Congress mjini Washington, Januari 6, 2021

 

Zaidi ya wabunge 30 wa chama cha Democratic wamewataka maafisa usalama na polisi wa Baraza la Congress la nchi hiyo wakusanye taarifa zote za watu waliokuwepo kwenye eneo hilo siku moja kabla ya kuvamiwa na magenge ya Donald Trump.

Wakati mabaraza mawili ya Congress - lile la wawakilishi la lile la seneti - yalipokuwa na kikao cha pamoja Jumatano, tarehe 6 Januari 2021 kwa ajili ya kupasisha ushindi wa urais wa Joe Biden wa uchaguzi wa Novemba 3, 2020, magenge ya rais wa Marekani, Donald Trump yalivamia jengo la Congress na kuua watu wasiopungua watano mbali na uharibifu mwingine. Hata Trump naye ana kesi ya kujibu.

Tags