Feb 20, 2021 07:51 UTC
  • Pentagon: Wanajeshi wa Marekani wataendelea kuhudumu huko Afghanistan

Katika hali ambayo serikali iliyotangulia ya Washington iliahidi kuwa, wanajeshi wa Marekani wataondoka Afghanistan hadi kufikia mwezi Mei mwaka huu; Mkuu wa Wizara ya Ulinzi ya Marekani (Pentagon) ametangaza kuwa bado uamuzi haujachukuliwa kuhusu suala hilo na hivi sasa wanajeshi wao wanaendelea kuwepo huko Afghanistan.

Lloyd Austin Waziri wa Ulinzi wa Marekani ameashiria kile alichokitaja kuwa machafuko na ukosefu wa amani nchini Afghanistan na kutaka kupunguzwa machafuko hayo na kuendelea mazungumzo ya amani kati ya serikali ya Kabul na kundi la wanamgambo wa Taliban kabla ya kuondoka nchini humo wanajeshi wa nchi ajinabi.  

Kikao cha Mawaziri wa Ulinzi wa Muungano wa Kijeshi wa Nchi za Magharibi (Nato)  kilifanyika juzi Alhamisi huko Brussels hata hivyo kilimalizika bila ya kufikiwa maafikiano kuhusu suala la Afghanistan. Lloyd Austin ameongeza kuwa, Marekani haitatoka Afghanistan haraka ili kuvihatarisha vikosi vya Nato. 

Mullah Badar Mkuu wa Timu ya Mazungumzo ya kundi la Taliban hivi karibuni alitaka Marekani iheshimu mapatano iliyofikia na kundi hilo kuhusu kuondoka wanajeshi wake huko Afghanistan na kutahadharisha kuwa Taliban haitavumilia uingiliaji wa nchi ajinabi nchini humo.  

Mullah Baladar, Mkuu wa Timu ya mazungumzo ya Taliban 

 

Tags