Amnesty International: Hali ya haki za binadamu Canada inatia wasiwasi
https://parstoday.ir/sw/news/world-i71450-amnesty_international_hali_ya_haki_za_binadamu_canada_inatia_wasiwasi
Sera za kibaguzi zinazoshuhudiwa katika nchi za Magharibi zinaendelea kuzitia wasiwasi taasisi na jumuiya za kimataifa za kutetea haki za binadamu.
(last modified 2025-11-07T02:31:33+00:00 )
Jun 20, 2021 02:14 UTC
  • Amnesty International: Hali ya haki za binadamu Canada inatia wasiwasi

Sera za kibaguzi zinazoshuhudiwa katika nchi za Magharibi zinaendelea kuzitia wasiwasi taasisi na jumuiya za kimataifa za kutetea haki za binadamu.

Hivi karibuni mashirika ya kutetea haki za binadamu ya Human Rights Watch na Amnesty International yametoa ripoti yakisema kuwa: Kila mwaka nchi ya Canada inawafunga jela na katika mazingira ya kibaguzi maelfu ya watu wakiwemo vilema kwa kosa la uhajiri. Amnesty International imekemea hali mbaya ya wahamiaji na wahajiri katika mahabusu hizo za Canada na kueleza kuwa nyaraka zinaonesha kwamba, wahajiri wanafungwa pingu na minyororo magerezani na kunyimwa fursa na kuwa na mawasiliano na dunia ya nje ya mahabusu wanakoshikiliwa.   

Ripoti hiyo imetolewa huku ubaguzi wa kimbari, kidini na kikaumu ukiendelea kushuhudiwa kwa wingi katika jamii ya nchi za Magharibi hususan huko Canada na Marekani. Sera hizo za ubaguzi zimeshika kasi zaidi katika miaka ya karibuni kiasi kwamba, hata Waziri Mkuu wa Canada, Justin Trudeau amekiri kwamba ubaguzi unaisumbua jamii ya nchi hiyo, na kwamba suala hilo linapaswa komeshwa. 

Justin Trudeau

Kugunduliwa kaburi la mamia ya watoto wa Wacanada asili waliokuwa wakishikiliwa katika shule ya bweni ya Kikatoliki ya Kamloops Indian kwenye jimbo la British Columbia na vilevile mauaji ya familia ya Kiislamu katika mji wa London jimboni Ontario ni vielelezo hai vya ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu katika nchi za Magharibi. Sasa kumeibuka maudhui hii ya ubaguzi unaofanyika nchini Canada dhidi ya wahajiri na vilema au watu wenye mahitaji maalumu. Hii ni pamoja na kuwa, hujuma dhidi ya wahajiri na watu wenye asili ya Asia zimeongezeka sana katika nchi za Magharibi ikiwemo Canada hasa katika kipindi hiki cha maambukizi ya virusi vya corona. Kwa kadiri kwamba, ripoti ya makundi ya kutetea haki za kijamii nchini Canada inasema kuwa, ukatili wa kimbari dhidi ya Wamarekani wenye asili ya Asia hauhusu Marekani pekee bali katika miezi ya karibuni kumeshuhudiwa mashambulizi na hujuma dhidi ya Wasia wa Canada.   

Amy Go ambaye ni mkuu wa Baraza la Taifa la Uadilifu wa Kijamii la Wacanada wenye asili ya China ametangaza kuwa, hujuma na mashambulizi dhidi ya raia wenye asili ya Asia nchini Canada yaliongezeka sana mwaka jana kuliko hata Marekani.

Hii ni licha ya kuwa, Marekani, Canada na nchi za Magharibi kwa ujumla zimekuwa zikijigamba kuwa watetezi wa haki za binadamu na zinazituhumu nchi nyingine  kuwa zinakiuka na kukanyaga haki hizo. Mienendo mibaya na ya kikatili ya raia wazungu wa nchi hizo za Magharib na hata polisi na wanasiasa wao dhidi ya raia wenye asili ya Afrika, Asia, Wahindi Wekundu, jamii za wafuasi wa dini za wachache kama Waislamu, wanawake na kadhalika, na ubaguzi unaoshuhudiwa katika sekta nyingi kama elimu, ajira na masuala mengine ya kijamii vimeanika na kuweka wazi uongo wa nchi hizo katika madai yao ya kutetea haki za binadamu.

Mambukizi ya virusi vya corona na haja ya wahajiri na jamii za wachache ya kupewa chanjo na matibabu ya corona katika nchi hizo za Magharibi vimefichua sura nyingine ya ubaguzi mkubwa na uliokita mizizi katika nchi hizo. Katika baadhi ya nchi hizo raia wenye asili ya Afrika huwekwa mwishoni kabisa kwenye safu ya watu wanaopewa huduma ya matibabu na chanjo ya corona na wengi wao hufariki dunia kutokana na kutelekezwa na kutopewa huduma za matubabu wakati mwafaka. Gavana wa Illinois huko Marekani anasema kuhusu suala hilo kwamba: Ni vigumu sana kuweza kufidia makumi au huenda karne kadhaa za ukosefu wa usawa na dhulma iliyofanyika kwa raia weusi katika masuala ya huduma za tiba.

Katika hali hii inaonekana kuwa, viongozi wa nchi za Magharibi wanalazimika kutzama upya sera na siasa zao na kufanya jitihada kubwa za kurekebisha mienendo yao kuhusiana na jamii za waliowachache hususan raia wenye asili ya Afrika na Asia katika nchi hiyo.