Ripoti: Canada inakiuka sheria za kimataifa kwa kuiuzia silaha Saudi Arabia
Ripoti mpya ya mashirika ya kimataiafa ya kutetea haki za binadamu imeitaka serikali ya Waziri Mkuu wa Canada, Justin Trudeau isimamishe kuuuzia silaha utawala wa Saudi Arabia ikisisitiza kuwa, mauzo hayo si tu yanakiuka haki za binadamu, lakini pia yanavunja sheria za kimataifa.
Ripoti hiyo iliyotolewa jana Jumatano na mashirika ya Amnesty International Canada na Project Ploughshares ina anuani isemayo "Hakuna Ushahidi Wenye Itibari; Tathmini ya Kosa la Canada Kuiuzia Silaha Saudi Arabia."
Katika ripoti hiyo, mashirika hayo ya kutetea haki za binadamu yamemtaka Waziri Mkuu Justin Trudeau asitishe mara moja uuzaji silaha wa serikali ya Ottawa kwa utawala wa Saudi Arabia, yakisisitiza kuwa mauzo hayo yanakwenda kinyume na Hati ya Mauzo ya Silaha (ATT), mkataba wa kimataifa ambao Canada ilijiunga nao mwaka 2019.
Mashirika hayo ya kimataifa ya kutetea haki za binadamu yamesema katika ripoti hiyo kuwa, yumkini silaha hizo zinatumiwa na utawala wa Aal Saud kukiuka sheria za kimataifa za haki za binadamu dhidi ya wananchi wa Yemen wakiwemo wanawake na watoto wasio na hatia yoyote.
Ikipata uungaji mkono wa Marekani, Imarati na nchi nyingine kadhaa, Saudi Arabia, ilianzisha vita dhidi ya Yemen mwezi Machi 2015 na kuiwekea nchi hiyo mzingiro wa angani, baharini na nchi kavu.
Mashirika ya kutetea haki za binadamu na jumuiya za kiraia za ndani na nje ya Canada kwa muda sasa zimekuwa zikimshinikiza Waziri Mkuu wa nchi hiyo Justin Trudeau ili asimamishe kuuuzia silaha utawala wa Saudi Arabia unaofanya jinai kila leo dhidi ya wananchi wa Yemen.
Hii ni katika hali ambayo, Waziri Mkuu huyo wa Canada huko nyuma aliahidi kuangalia upya uuzaji silaha wa serikali ya Ottawa kwa utawala wa Saudi Arabia, lakini mpaka leo hii hajatekeleza kivitendo ahadi hiyo.