Canada kuwanyima mishahara wafanyakazi wanaokwepa chanjo ya UVIKO-19
https://parstoday.ir/sw/news/world-i75490-canada_kuwanyima_mishahara_wafanyakazi_wanaokwepa_chanjo_ya_uviko_19
Serikali ya Canada imeanzisha sheria mpya kali za kupambana na watu wanaofanya ukaidi wa kudunga chanjo za UVIKO-19 ambazo zitawaathiri watu wengi.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Oct 07, 2021 11:51 UTC
  • Canada kuwanyima mishahara wafanyakazi wanaokwepa chanjo ya UVIKO-19

Serikali ya Canada imeanzisha sheria mpya kali za kupambana na watu wanaofanya ukaidi wa kudunga chanjo za UVIKO-19 ambazo zitawaathiri watu wengi.

Katika sheria zake hizo mpya na kali, serikali ya Canada imetangaza kuwa, kila mfanyakazi wa serikali, afisa wa polisi na taasisi za kijeshi ambaye hajapiga chanjo ya corona, atakatiwa mshahara.

Shirika la habari IRNA limeripoti habari hiyo na kuongeza kuwa, siasa hizo za kuwalazimisha wananchi wa Canada kupiga chanjo ya UVIKO-19 zimechukuliwa kwa amri ya moja kwa moja ya waziri mkuu wa nchi hiyo, Justin Trudeau na zitawaathiri takriban wafanyakazi laki tatu wa serikali.

Waziri Mkuu wa Canada ameonya kwamba, hatua kali zinawasubiri wafanyakazi wa serikali ambao wanatoa taarifa za uongo kuhusu hali yao ya chanjo.

Wasafiri wote wanaoingia Canada sasa watatakiwa wawe wamepiga chanjo kamili ya corona

 

Vile vile wasafiri wote wenye umri wa miaka 12 na kuendelea  wanaoingia Canada kwa njia ya anga na treni, hawatoruhusiwa kuingia nchini humo ila baada ya kuwa wamepiga chanjo kamili ya UVIKO-19. Sheria hiyo itaanza kutekelezwa mwishoni mwa mwezi ujao wa Novemba.

Justin Trudeau ameongeza kuwa, katika kipindi cha wiki chache zijazo, serikali yake itatangaza pasipoti ya chanjo ya corona kwa ajili ya wasafiri wa kimataifa na hatua kali zitachukuliwa kwa yeyote atakayetoa vitisho au kuwasumbua maafisa wa afya watakaokuwa wanawauliza wasafiri pasi hizo.

Zaidi ya asilimia 82 ya raia wa Canada wenye umri wa kuanzia miaka 12 na kuendelea wameshapiga chanjo kamili ya corona na asilimia 88 ya raia wa nchi hiyo wameshapiga angalau chanjo moja.