Russia yaitaka Misri iimarishe usalama katika viwanja vyake vya ndege
Russia imeitaka Misri ihakikishe imeimarisha usalama katika viwanja vyake vya ndege hadi mwishoni mwa nusu ya kwanza ya mwaka huu wa 2016.
Shirika la habari la Itar-Tass la Russia limemnukuu Valery Ukulov, naibu waziri wa usafiri na uchukuzi wa nchi hiyo akisema jana Jumatano kuwa, viwanja vya ndege ya Misri vimeahidi kuwa hadi kufikia mwishoni mwa miezi sita ya awali ya mwaka huu wa 2016 vitakuwa vimeshatimiza masharti ya kiusalama yanayotakiwa na Russia.
Okulov amesema, wataalamu wa masuala ya kiusalama wa Russia wamewapendekezea maafisa wa Misri mambo kadhaa kwa ajili ya kuimarisha usalama katika viwanja vya ndege vya nchi hiyo.
Siku ya Jumanne pia, Waziri wa Usafiri na Uchukuzi wa Russia, Maxim Sokolov alisema kuwa, wizara yake hadi hivi sasa haijapokea majibu yoyote kuhusiana na mashtaka ya mashirika ya ndege ya Russia kuhusu usalama mdogo katika viwanja vya ndege vya Misri.
Ikumbukwe kuwa, mwisho mwa mwezi Oktoba mwaka jana, ndege moja ya abiria ya Russia ilianguka katika jangwa la Sinai la Misri, na Moscow ikasimamisha safari za ndege zake za abiria kuelekea Misri baada ya kugundulika kuwa ndege hiyo iliripuliwa kwa bomu.