UNICEF: Ukiukaji wa haki za watoto umekithiri duniani
(last modified Sat, 01 Jan 2022 03:33:10 GMT )
Jan 01, 2022 03:33 UTC
  • UNICEF: Ukiukaji wa haki za watoto umekithiri duniani

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia Watoto UNICEF limesema mwaka uliomalizika wa 2021 umekuwa wa machungu na ukiukwaji mkubwa wa haki za watoto katika mizozo ya muda mrefu na ile mipya iliyojitokeza katika nchi mbalimbali duniani.

Taarifa iliyotolewa na shirika hilo imesema, kuanzia Afghanistan hadi Yemen, Syria hadi kaskazini mwa Ethiopia, maelfu ya watoto wamekuwa waathirika wakati huu ambapo mizozo ya kivita, mapigano ya kikabila na ukosefu wa usalama vikiendelea kushamiri.

“Wiki iliyopita tu, watoto wanne waliripotiwa kuwa miongoni mwa watu 35 waliouawa huko jimboni Kayan nchini Myanmar. Hii ni moja ya mifano dhahiri ya karibuni zaidi ya jinsi mizozo inavyogharimu uhai wa mtoto sambamba na vitisho kwa wafanyakazi wanaotoa huduma za kibinadamu..” imesema sehemu ya taarifa hiyo.

Mkurugenzi Mkuu wa UNICEF, Henrietta Fore akinukuliwa kwenye taarifa hiyo amesema "mwaka hadi mwaka, pande katika mizozo zimeendelea kuonesha kupuuza haki na ustawi wa watoto. Watoto wanasumbuka, watoto wanakufa kwa sababu ya ukatili. Kila juhudi lazima ifanyike ili kuepusha watoto na majanga.”

Watoto katika maeneo ya vita

Huku taarifa hiyo ikiashiria kuwa takwimu za mwaka mzima uliomalizika wa 2021 zikiwa bado hazijatoka, takwimu za mwaka wa kabla yake wa 2020 zinaonesha ukikukwaji mkubwa wa haki za watoto uliothibtishwa na Umoja wa Mataifa.

Taarifa hiyo inasema matukio ya utekaji nyara watoto yalithibitishwa kwa kiwango cha juu katika nchi za Somalia, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, pamoja na nchi za ukanda wa ziwa Chad ambazo ni Chad, Nigeria, Cameroon na Niger.

Kwa upande wa vitendo vilivyothibitishwa vya ukatili wa kingono dhidi ya watoto vilikuwa vingi zaidi Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Somalia na Jamhuri ya Afrika ya Kati.

Mkurugenzi Mkuu wa UNICEF, Henrietta Fore amemalizia taarifa yake hiyo kwa kusema: “hatimaye watoto wanaoishi kwenye mazingira ya kivita watakuwa salama pale tu pande kwenye mzozo zitakapochukua hatua kulinda watoto na kuacha kufanya vitendo vya ukatili. Tunapofunga mwaka 2021 natoa wito kwa pande zote kwenye mizozo kuacha mashambulizi dhidi ya watoto, zizingatie haki za watoto na kusaka suluhu ya kisiasa kumaliza vita”.../