Ripoti: China inaimarisha silaha za nyuklia kukabiliana na tishio la Marekani
Imedokezwa kuwa China imeongeza kasi ya upanuaji wa silaha zake za nyuklia baada ya tathmini mpya kuhusu tishio la Marekani kwa nchi hiyo.
Gazeti la Wall Street Journal limedai katika ripoti yake kuwa, kuhusika Marekani katika mgogoro wa Ukraine kumeifanya Beijing isisitize suala la kuimarisha uwezo wa kujihami, na hivyo imeamua kujenga maghala mapya 100 ya makombora ambayo yanaweza kusheheni silaha za nyuklia.
Ripoti hiyo inanukuu duru zikisema kuwa, viongozi wa China wanaamini kwamba kuimarisha zana zao za nyuklia kutaizuia Marekani kujiingiza vitani moja kwa moja katika eneo la China Taipei ambalo ni chanzo cha mgogoro baina ya China na Marekani.
Wizara ya Ulinzi ya Marekani inadai kuwa ifikapo mwaka 2030, China itakuwa na mabomu 1,000 ya nyuklia. Marekani yenyewe ina mabomu 3,750 ya nyuklia katika maghala yake.

Hata hivyo China imekanusha taarifa kuwa inalenga kupanua uwezo wake wa silaha za nyuklia huku ikisisitiza kuwa kile inacholenga ni kuwa na uwezo wa kutosha wa kulinda maslahi yake ya usalama wa taifa.
Mkurugenzi wa Idara ya Udhibiti wa Silaha katika Wizara ya Mambo ya Nje ya China, Fu Cong, alisema mapema mwaka huu kuwa, madai ya Marekani kuwa China inapanua uwezo wake wa silaha za nyuklia hayana ukweli wowote.
Marekani na China zimekuwa zikizozana kuhusu eneo la China Taipe ambalo linajulikana pia kama Taiwan. China inasisitiza kuwa eneo hilo ni sehemu ya ardhi yake, huku Marekani ikiunga mkono na kuchochea eneo hilo kujitenga na China.